Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametangaza kufungamana na familia za raia wa Burkina Faso ambao waliuawa katika hujuma ya kigaidi hivi karibuni.
Katika taarifa leo Jumatatu, Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha masikitiko yake makubwa kutokana na kupoteza maisha raia wa Burkina Faso katika hujuma ya makundi ya kigaidi. Amesema chimbuko la ugaidi ni kuwa baadhi ya nchi zinaona maslahi yao yako katika kuibua hali ya kukosekana usalama na uthabiti.
Siku ya Alhamisi watu wasiopungua 44 waliuawa katika mashambulizi mawili ya kigaidi magharbi mwa Burkina Faso.
Serikali ya Burkina Faso imelaani vikali hujuma hiyo na kutangaza Jumapili na Jumatatu kuwa siku za maombolezo ya kitaifa.
Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi. Burkina Faso katika miaka ya karibuni imekumbwa na mashambulizi kadhaa ya umwagaji damu.
Mashambulio hayo awali yalianzia upande wa kaskazini mwa nchi hiyo na kisha kuendelea mashariki na katikati mwa nchi hiyo. Kuanzia mwaka 2015 hadi sasa mamia ya watu wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi huko Burkina Faso. Akthari ya mashambulio hayo yamejiri katika maeneo ya mpakani kati ya Burkina Faso na Mali, Niger na Benin.
Hivi karibuni wananchi waliokuwa na hasira Burkina Faso waliuzuia msafara wa jeshi la Ufaransa uliokuwa unapita nchini humo kuelekea Mali wakisema kuwa pamoja na kuwepo askari hao wa kigeni eneo hilo linashuhudia hujuma za kigaidi. Baadhi ya waandamanaji walisisitiza kuwa msafara huo wa Ufaransa ulikuwa unawapelekea silaha magaidi wakufurishaji.