IRGC yashambulia tena ngome za magaidi Kurdistan ya Iraq

Kwa mara nyingine, Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeshambulia na kuharibu ngome za magaidi katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan, kaskazini mwa Iraq.

Shirika la habari la Fars News limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Kikosi cha Nchi Kavu cha jeshi la IRGC kimeanzisha wimbi jipya la operesheni hiyo dhidi ya makundi ya kigaidi kwa kutumia makombora, droni na maroketi.

Jeshi la SEPAH limefanya operesheni hiyo huku Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Hamzah Sayyid al-Shuhada cha IRGC akisema kuwa, vyombo vya usalama vya Iran vimewatia mbaroni maajenti 100 wa makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga.

Brigedia Jenerali Mohammad Taqi Osanlou amesema maafisa usalama wa Iran wamefanikiwa kuzima njama za maadui za kupenyeza silaha nchini kupitia mpaka wa kaskazini magharibi.

Baadhi ya magaidi hao waliotiwa mbaroni ni wanachama wa genge la kigaidi la Komala na kundi la Wakurdi linalojiita Democratic Party of Iranian Kurdistan (PDKI). Makundi haya yamehusika pakubwa katika kukoleza moto wa fujo na ghasia nchini Iran.

Tokea Septemba 24, wanajeshi wa IRGC wamekuwa wakishambulia ngome na maficho ya magenge ya kigaidi katika eneo la Kurdistan ya Iraq. Aidha Mei mwaka huu, Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lililenga na kusambatarisha ngome za magaidi hao katika eneo hilo la Iraq lenye mamlaka ya ndani.

SEPAH inasisitiza kuwa, oparesheni hizo zitaendelezwa kwa nguvu zote hadi vitisho vilivyopo vitakapozimwa kikamilifu na ngome za magenge ya kigaidi zitakapoondolewa; na hadi pale viongozi wa Erbil watakapochukua hatua dhidi ya magaidi hao wanaotishia amani na usalama wa Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *