Afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameeleza kuwa, jinai ya kumuua shahidi Ammar Mefleh ni jinai ya kivita na dhidi ya binadamu na haitasalia bila jibu.
Mwanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel juzi Ijumaa alikabiliwa na muqawama wakati alipojaribu kumtia nguvuni Ammar Mefleh katika kitongoji cha Huwara katika mji wa Nablus; ambapo alimmiminia risasi kadhaa kijana huyo Mpalestina na kumuua shahidi kikatili.
Televisheni ya al Masira imeripoti kuwa, Ismail Ridhwan afisa wa ngazi ya juu wa Hamas amesisitiza kuwa, utawala ghasibu utajuta kwa kutenda jinai hiyo kwa sababu, mauaji hayo ya kinyama yamejeruhi hisia za wananchi wote wa Palestina.
Ridhwan ameyataka makundi yote ya muqawama ya Palestina popote pale kumsaka na kumuangamiza Mzayuni aliyetenda jinai hiyo ya kutisha. Ameongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel unapasa kujua kwamba utagharamika pakubwa kutokana na jinai zake za kila uchao dhidi ya raia wa Palestina.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas amesisitiza kuwa, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unapasa kuwawashia moto Wazayuni Maghasibu kwa jinai zao za kila siku dhidi ya Wapalestina.
Ridhwan ametilia mkazo akisema: Utawala wa Kizayuni unaoukalia kwa mabavu mji wa Quds unajaribu kupotosha fikra za waliowengi kwa kuhalalisha jinai unazotenda huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan; hata hivyo jinai hizo zitakabiliwa na jibu kutoka Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, al-Quds na katika ardhi zilizovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1948. “Tunawaomba Wapalestina wote kujibu mauaji ya Mefleh”,amesema Ismail Ridhwan.