Israel yakiri kuwa wazayuni 29 wameangamizwa katika mwaka unaomalizika wa 2022

Idara ya usalama wa ndani ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Shabak imekiri kuwa, Wazayuni 29 waliuawa katika operesheni za mashambulizi zilizofanywa na Wapalestina katika mwaka huu unaomalizika wa 2022.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Shabak, hadi kufikia leo, Wapalestina wametekeleza operesheni 1933, ambapo Wazayuni 29 wameuliwa na wengine 128 wamejeruhiwa, likiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa gazeti la Yediot Aharonot, ongezeko kubwa la operesheni za mashambulio za Wapalestina limewatia wasiwasi makamanda wa usalama wa Israel.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Kizayuni licha ya Wapalestina kutiwa nguvuni kwa wingi na askari wa utawala haramu wa Israel katika maeneo mbalimbali ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, operesheni dhidi ya Wazayuni zimeongezeka, na kundi jipya lijulikanalo kama “Arin al-Usud” limetangaza kuwepo kwake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ongezeko kubwa la operesheni za mashambulio na kushindwa Shabak kuzima operesheni zisizopungua 460 tangu ulipoanza mwa mwaka huu hadi sasa kumezikanganya duru za usalama za utawala wa Kizayuni.

Wakati huo huo duru za Palestina zimetangaza kuwa, mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa muqawama na kusisitiza kwamba, katika mwaka huu zimetekelezwa operesheni 14,000 dhidi ya Wazayuni ambapo Wazayuni 31 wameangamizwa.
Duru hizo za Palestina zimeeleza pia kwamba, Wapalestina 221 wameuliwa shahidi na utawala wa Kizayuni, 167 kati yao katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu, 50 katika Ukanda wa Gaza na wanne wengine katika ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *