Israel yapuuza amri ya ICJ, nakuendelea kumwaga damu za Wapalestina Gaza

Utawala haramu wa Israel umedharau uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuutaka uchukue hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, na badala yake jeshi la utawala huo pandikizi limeendelea kumwaga damu za Wapalestina wa Gaza.

Shirika rasmi la habari la Palestina la WAFA limenukuu duru za matibabu leo Jumamosi zikisema kuwa, Hospitali ya Mashahidi ya al-Aqsa katikati ya Gaza imepokea idadi kubwa ya miili na watu waliojeruhiwa, baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni kushadidisha mashambulizi ya anga katika mji wa Deir al-Balah.

Habari zaidi zinasema kuwa, raia tisa, wakiwemo wanawake wameuawa shahidi baada ya ndege za kivita za utawala katili wa Israel kushambulia kwa mabomu majengo kadhaa ya makazi ya raia katika mji wa Khan Younis, kusini mwa Gaza.

Aidha watu wengine kadhaa wameripotiwa kuuliwa shahidi na kujeruhiwa katika hujuma hizo za anga za Israel katika eneo la al-Geneina, mashariki mwa Rafah.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, kwa akali Wapalestina 183 wameuawa shahidi huku wengine zaidi ya 377 wakijeruhiwa katika muda wa saa 24 zilizopita, katika mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo lililozonigirwa.

Wazayuni wameshadidisha umwagaji damu za Wapalestina katika hali ambayo, jana Ijumaa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iliiamuru Israel iache vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema katika taarifa kuwa: Njia pekee ya kutekeleza uamuzi wa muda wa Mahakama ya Kimataifa ya ICJ ni kusitisha vita.

Aidha imekosoa ukweli mchungu kwamba, hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya juu wa Israel, akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliyeahidi kuheshimu hukumu hiyo, na badala wake wametangaza kuendelea kwa mashambulizi hayo ya kinyama ya ‘kuusambaratisha kikamilifu’ Ukanda wa Gaza.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *