Utawala haramu wa Israel umepinga ombi la Marekani la kuutaka uipe Ukraine makombora na silaha nyinginezo, baada ya Russia kuonya vikali dhidi ya kupewa Kiev misaada ya kijeshi na zana za vita.
Tovuti ya Russia Today imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, duru za habari zimenukuliwa na shirika la habari la Axio zikisema kuwa, Israel imedaiwa kukataa ombi hilo la US la kuipa Ukraine makombora ya ardhini hadi angani na mifumo yake chakavu ya makombora ya Hawk.
Duru za habari zinaarifu kuwa, Washington iliwasiliana na Israel wiki mbili zilizopita kuhusu ombi hilo la kuutaka utawala huo wa Kizayuni uipe Ukraine silaha zake zilizopitwa na wakati, ulizouziwa na Marekani miaka ya 60.
Baada ya onyo kali la Russia, Wizara ya Vita ya Israel imeingiwa na kiwewe na kutoa taarifa iliyodai kuwa, sera ya Tel Aviv ya kutoipa Ukraine silaha haijabadilika.
Hii ni katika hali ambayo, gazeti la New York Times liliripoti hivi karibuni kuwa, Marekani inatuma kimya kimya mamia kwa maelfu ya makombora ya mizinga nchini Ukraine kutoka kwenye maghala inayodai ni yake ya dharura yaliyo katika utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, maafisa wa Marekani wamekuwa wakifanya kazi nyuma ya pazia kukusanya makombora ya kutosha ili kuifanya Ukraine ijizatiti vya kutosha na silaha mwaka huu 2023.
Hata hivyo serikali ya Moscow imeonya kwamba, uamuzi huo wa kuisheheneza silaha Ukraine utajibiwa vikali na Russia na kwamba Moscow nayo itatumia silaha kali zaidi za kukabiliana na silaha hizo za Magharibi.