Israel yawakatia maji Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi

Utawala haramu wa Israel umewafungia maji mamia ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Shirika la habari la Palestine al-Yaum limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, jana Alkhamisi askari wa Kizayuni waliharibu bomba pekee la kusambaza maji kwa wakazi wa al-Auja, kaskazini mwa mji wa kale wa Jericho, na hivyo kuwafanya Wapalestina zaidi ya 1,200 wa eneo hilo kukosa maji safi.

Hasan Mleihat, Msimamizi wa Shirika la Kulinda Haki za Mabedui la al-Baidar amesema, al-Auja ni moja ya jamii kubwa zaidi katika Ukingo wa Magharibi, na wakazi wake wamekuwa wakilengwa na hujuma za askari wa Kizayuni na walowezi wa Kiyahudi.

Huku mamia ya Wapalestina hao wa al-Auja wakikubwa na ukosefu mkubwa wa maji ya kunywa, walowezi wa Kizayuni wanaolizunguka eneo hilo wana maji ya kutosha ambayo wanayatumia mashambani na hata kuosha magari yao.

Hii si mara ya kwanza kwa utawala haramu wa Kizayuni kuwafungia maji Wapalestina, ikiwa ni sehemu ya jinai ambazo zinafanywa na utawala huo pandikizi kwa lengo la kuwashinikiza Wapalestina hao kusalimu amri mbele ya utawala huo khabithi.

Vitendo hivyo vya kinyama sambamba na vile vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *