Kamisheni ya Wafungwa wa Kipalestina imesema utawala haramu wa Israel umewaweka watoto zaidi ya 600 wa Kipalestina katika kifungo cha nyumbani, tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, huku utawala huo wa Kizayuni ukiendelea na kampeni yake ya kuwanyanyasa na kuwatia mbaroni Wapalestina.
Tume hiyo ya kupigania maslahi ya wafungwa wa Kipalestina imesema katika taarifa ya jana Jumatatu kuwa, utawala wa Kizayuni umeshadidisha mbinu hiyo ya kuwawekea mbinyo watoto wadogo na vijana hususan huko mashariki mwa mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds, katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, Israel imekiuka sheria yake mwenyewe inayopiga marufuku kufungwa jela au kuzuiliwa watoto wenye chini ya miaka 14, na watoto wa Kipalestina waliowekwa chini ya kifungo cha nyumbani wanavishwa bangili maalum za kuwafuatilia, na hawaruhusiwa kwenda shule.
Kwa mujibu wa Klabu ya Wafungwa wa Kipalestina (PPC), wanajeshi wa Israel wamewatia mbaroni Wapalestina 6,500 wakiwemo watoto zaidi ya 800 katika eneo lote la Ukingo wa Magharibi linaokaliwa kwa mabavu tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
PPC ilisema wafungwa wote wa Kipalestina wanazuiliwa katika mazingira ya kinyama, hawapati huduma muhimu za kimatibabu, na wanatelekezwa kwa makusudi.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliutaka Umoja wa Mataifa uliweke jina la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwenye orodha ya tawala wauaji wa watoto.