Jamhuri 2023: Mudavadi Akaribisha Wageni Ikulu Ya Rais Badala Ya Gachagua

ITIFAKI za urais (presidency) wakati wa maadhimisho ya Jamhuri Dei 2023 zilionekana kukiukwa kutokana na jinsi viongozi wakuu serikalini walivyoondoka Bustani ya Uhuru, Nairobi.

Kama ilivyo desturi, baada ya kiongozi wa nchi kuhutubu, huondoka rasmi kisha anafuatwa na mkewe – mama wa taifa, halafu naibu wake.

Rais William Ruto alipohitimisha hotuba yake kwa taifa, alifuatwa na mkewe, Bi Rachael Ruto kisha akafuatwa na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi.

Kulingana na mfawidhi (MC), msafara wa Bw Mudavadi ulipaswa kufuata wa Mama Taifa ikisemekana “aliratibiwa kukaribisha wageni kule Ikulu, Jijini Nairobi”.

Naibu Rais, Rigathi Gachagua alifuata msafara wa Bw Mudavadi.

Utaratibu huo unaibua maswali kuhusu itifaki za urais na uongozi hasa katika hafla za kitaifa.

Akiondoka Uhuru Gardens, Dkt Ruto alisindikizwa na Mabw Mudavadi, Gachagua na Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja.

Maadhimisho ya Jamhuri 2023 ambayo yaliongozwa na Dkt Ruto, yalihudhuriwa na wageni mashuhuri kutoka nje ya nchi, wakiwemo; Rais wa Zanzibar (Tanzania) Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Ethiopia, Sahle Work Zewde.

Wengine ni Makamu wa Rais Burundi, Prosper Bazombanza, Naibu Waziri Mkuu Uganda Rebecca Kadaga ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hafla hiyo ya Kenya kuadhimisha miaka 60 baada ya kupata uhuru wa kujitawala, pia ilihuhduriwa na mabalozi.

Katika siku za hivi karibuni, Bw Mudavadi ameonekana kumwakilisha Rais Ruto ziara kadha wa kadha nje ya nchi.

Hatua hiyo inaibua maswali kuhusu uhusiano wa Rais Ruto na naibu wake.

Gachagua, hata hivyo, amekuwa akidai kwamba yeye na rahisi wangali pamoja.

Wakati mmoja alinukuliwa akihoji kwamba yeye hutumwa nje ya nchi haja inapoibuka, na furaha yake ni kuona anasalia nchini kuhudumia Wakenya.

Bw Gachagua, maarufu kama Riggy G, hujiita ‘mtu wa mkono wa Rais William Ruto’.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *