Mafuriko yaliyoikumba nchi ya Somalia yamesababisha hasara kubwa kwa nchi hiyo iliyoko katika Pembe ya Afrika.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema mafuriko yaliyosababishwa na mvua za msimu Somalia, yamesababisha uharibifu huku nyumba za makazi na mashamba vikisombwa na maji na vituo vya afya vikilazimika kufungwa.
Stephane Dujarric amesema kuwa, kwa mujibu wa makadirio ya awali, watu wasiopungua watano wamefariki dunia na zaidi ya wengine 460,000 wameathiriwa na mafuriko hayo.
Kadhalika watu wapatao 219,000 wakiwemo pia wanawake na watoto wamelazimika kuyahama makazi yao.
Uharibifu mkubwa umeshuhudiwa katika jimbo la kati la Hiiraan huko Hirshabelle ambapo maelfu ya watu wamehamishiwa huko Beledweyne.
Dujarric amesema ikiwa mvua zitaendelea nchini Somalia, wanakadiria kuwa hadi watu milioni 1,6 wanaweza kuathiriwa na mafuriko.
Mafurikko hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, kwa miezi kadhaa sasa Somalia imekuwa ikitaabika kwa ukame mbaya kabisa ambao haujawahi kushuhudiwa katikka miongo ya hivi karibuni na kutishia uhai wa mamilioni ya watu.
Janga la mafuriko linaripotiwa nchini Somalia siku chache tu baada ya mataifa kadhaa ya Afrika Mashariki kukumbwa pia na mafuriko. Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda ni mataifa ambayo hivi karibuni baadhi ya maeneo ya mataifa hayo yalikumbwa na mafuriko na maporomoka ya udongo na kusababisha mamia ya watu kufariki dunia.