Janga la moto laua wanafunzi 17 Kenya, Rais Ruto aagiza uchunguzi ufanywe haraka

Rais Willam Ruto wa Kenya ametoa amri ya kufanyika uchunguzi haraka iwezekanavyo kuhusiana na tukio la moto lililotokea katika Skuli ya Msingi ya Endrasha katika Kaunti ya Nyeri na kusababisha wanafunzi 17 kupoteza maisha na wengine 14 kujeruhiwa vibaya.

Vyombo vingi vya habari vya ndani na nje ya Kenya vimeiripoti kwa wingi habari ya moto huo kama ambavyo vingine vimemnukuu Rais Willam Ruto akisema: “Tunazifariji familia za watoto waliopoteza maisha yao katika mkasa wa moto kwenye shule ya Hillside Endarasha Academy Kaunti ya Nyeri. Nimeiagiza Wizara ya Usalama wa Ndani kufanya juhudi zake zote kuzisaidia familia zilizoathirika.”

Msemaji wa kitengo cha Huduma ya Taifa ya Polisi, Daktari Resila Onyango amesema kuwa, timu ya maafisa wa uchunguzi imetumwa katika skuli hiyo iliyoko eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri.

Aidha amesema: “Wanafunzi kumi na sita wamechomeka kiasi cha kutotambuliwa huku mmoja akifariki dunia wakati akipelekwa hospitalini. Tunachunguza kilichosababisha moto huo na tutachukua hatua zinazohitajika.”

Timu ya wachunguzi inaongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai wa Kenya (DCI), John Onyango, na maafisa kutoka Afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Dk Resila Onyango amesema: “Moto ulizuka katika bweni, Ulizuka usiku na bado hatujabaini kilichousababisha.”

Kwa upande wake, televisheni ya KTN ya Kenya imesema kuwa, wanafunzi 14 waliowahishwa hospitalini wana hali mbaya, suala ambalo linaleta hofu ya kuongezeka idadi ya vifo vilivyotokana na moto huo.

Katika sehemu nyingine, Msemaji wa Jeshi la Polisi la Kenya, Resila Onyango amesema kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Tunawaombea dua waliojeruhiwa wapone haraka. Mawazo na fikra zetu ziko kwa familia za watoto wambao wamepoteza maisha katika janga hilo la moto.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *