Japan imetangaza kuwa inaunga mkono pendekezo la kupewa uanachama Umoja wa Afrika (AU) katika kundi la G20.
Hayo yalisemwa jana Jumatatu na Fumio Kishida, Waziri Mkuu wa Japan na kueleza kuwa, nchi hiyo itaunga mkono wazo la AU kupewa uanachama katika jumuiya hiyo kubwa zaidi ya kiuchumi duniani.
Viongozi wa Afrika wamekuwa wakilalamikia kutengwa na kutojumuishwa bara hilo katika taasisi muhimu duniani kama G20 na uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya mchango wake mkubwa katika ustawi wa uchumi wa dunia.
AU inapania kujiunga na G20 wakati huu ambapo nchi za Magharibi zinaendeleza kampeni kubwa za kutaka kutimuliwa Russia katika jumuiya hiyo ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani.
Afrika Kusini ndio nchi pekee ya Afrika mwanachama kundi hilo la G20, ambalo linadhibiti karibu asiliamia 80 ya uchumi wa dunia na kujumuisha thuluthi mbili ya idadi ya watu wote ulimwenguni.
Japokuwa nchi za Magharibi siku zote zimekuwa zikiliangalia bara la Afrika kwa jicho la kikoloni lakini kutokana na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama yaliyotokea ulimwenguni na katika kanda hiyo, sasa Afrika imepata umuhimu mkubwa na makhsusi katika mfumo wa kimataifa.
Nchi za bara hilo zimekuwa medani ya ushindani mkubwa wa kiuchumi na kiusalama baina ya madola makubwa ikiwemo Marekani, Russia, China na Ulaya.