Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesema Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinatambua vizuri kile ambacho kitawafika iwapo zitathubutu kutelekeza kivitendo vitisho vyao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, Msemaji wa Jeshi la Iran amesema ukongwe wa Rais Joe Biden na tabia yake ya kupenda kulala ndiyo imempelekea atumie lugha ya vitisho dhidi ya Iran.
Amewashauri Biden na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Yair Lapid watathmini matukio yaliyoshuhudiwa huko nyuma ya kushindwa na kudhalilishwa Marekani katika eneo hili la Asia Magharibi kabla ya kubwabwaja na kulitishia taifa la Iran.
Jenerali Shekarchi ameeleza kuwa, kutekwa pango la ujasusi la Marekani mjini Tehran, kuzikwa wanajeshi wa nchi hiyo katika jangwa la Tabas, kushindwa vikaragosi vya dola hilo la kibeberu katika vita vya miaka 8 dhidi ya Iran, kutimuliwa askari wa US nchini Afghanistan, kupingwa kwa makombora kambi yake ya kijeshi ya Ain al-Assad mjini Baghdad, kutunguliwa droni yake ya kisasa aina ya Global Hawk katika Ghuba ya Uajemi na kushindwa kwa madhila magaidi wa ISIS walioanzishwa na Washington nchini Iraq na Syria ni baadhi ya mifano hai ya vipigo dhidi ya Wamarekani katika eneo.
Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran amesisitiza kuwa: (Wamarekani na Wazayuni) wanafahamu fika gharama watakayolipa kwa kutumia istihali ya ‘kutumia nguvu (za kijeshi) dhidi ya Iran.
Juzi Jumatano, Biden mara tu baada ya kuwasili katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel alitoa kauli ya uropokaji na kusema kuwa, ikilazimu, Marekani itatumia nguvu za kijeshi kuizuia Tehran isipate silaha za nyuklia.