Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kupoteza matumaini adui katika medani ya kukabiliana ana kwa ana na Iran kijeshi na kusema: “Ni kwa sababu hii ndio adui ameanzisha vitisho katika mitandao ya intaneti, vita vya utambuzi na vita vya vyombo vya habari dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.”
Shirika la Habari la IRNA limemnukulu Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Bagheri akizungumza mkoani Bushehr kusini mwa Iran amesema: “Ni kwa msingi huo ndio Iran hivi karibuni imekuwa ikikabiliwa na aina mbali mbali za vitisho kutoka kwa adui kwa lengo la kuibua hali ya kupoteza matumaini na usumbufu miongoni mwa wananchi.”
Meje Jenerali Bagheri ameendelea kusema kuwa, wananchi wa Iran pamoja na kuwa wana matatizo yakiwemo ya uchumi lakini hawakubali kuhadaiwa na adui na wameweza kutafuatisha baina ya malalmiko halali na ghasia.
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria umuhimu wa uwezo wa eneo la Ghuba ya Uajemi kwa matazamo kijeshi na ulinzi na kusema umuhimu huu ndio uliopelekea Marekani iitishe Iran mara kadhaa kupitia Ghuba ya Uajemi.
Aidha amesema maadui wamekiri kuwa uwezo mkubwa wa makombora ya Iran umefanya kubakia kwao katika Ghuba ya Uajemi kuwe ni hatari kubwa lakini pamoja na hayo adui anaendeleza chokochko zake za kijeshi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuuingiza utawala wa Kizayuni katika Ghuba ya Uajemi.
Ikumbukwe kuwa mwishoni mwa mwezi Septemba, maeneo kadhaa ya Iran yalishuhudia kuanza fujo na ghasia ambapo katika siku za awali za fujo hizo, ilibainika wazi kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya kawaida na vya kisasa vya maadui vilikuwa na mipango maalumu ya uchochezi.
Katika fujo na ghasia hizo ambazo zilibadilika na kuwa ugaidi, watawala wa kisiasa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na vyombo vyao vya habari na halikadhalika vyombo vya habari vinavyopinga Mapinduzi ya Kiislamu vya lugha ya Kifarsi ambavyo vinaungwa mkono na madola ya magharibi na watifaki wao, vilianza kudai kuunga mkono haki za taifa la Iran na kufanya kila lililowezekana kuunga mkono ghasia na kuvuruga usalama wa taifa la Iran.
Taarifa ya pamoja ya Wizara ya Usalama ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imeashiria nafasi kubwa ya mashirika ya kijasusi ya kigeni ya kijasusi hususan CIA katika kuandaa ghasia za kivita nchini Iran.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, taarifa hiyo ilisema, “CIA ilichukua jukumu kuu” la kuchochea ghasia na ugaidi Iran huku ikishirikiana kwa karibu na mashirika ya kijasusi ya Uingereza, utawala wa Israel na Saudi Arabia.