Jeshi la Israel lakiri kuwa katika wakati mgumu wa kukabiliana na operesheni za wanamapambano wa Kiislamu

Baadhi ya duru za Kizayuni zimeripoti kuwa, licha ya jeshi la Israel kuvamia kila siku na mara kwa mara maeneo ya Wapalestina na licha ya kufanya ukatili mkubwa dhidi ya Wapalestina lakini limeshindwa kuzuia operesheni za wanamuqawama na wanamapambano wa Kiislamu.

Shirika la habari la Kizayuni la “Walla” limewanukuu baadhi ya maafisa wa kijeshi wa utawala huo pandikizi wakikiri kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 kumeshafanyika operesheni 100 za ufyatuaji risasi dhidi ya Wazayuni na kuzimwa operesheni nyingine 200 ambapo asilimia 80 ya operesheni hizo zimefanyika katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina za Jenin na Nablos.

Shirika hilo limesema, sababu kuu ya kuongezeka operesheni za wanamuqawama wa Palestina ni uungaji mkono wa makundi ya wanamapambano wa Kiislamu hasa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Jihad al islami, kwa makundi ya maeneo hayo ya Wapalestina na pia kuingizwa kimagendo silaha katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kupitia mpaka wa Jordan.

Wakati huo huo gazeti la al Ra’y al Yaum limeripoti kuwa, huko nyuma makundi ya Wapalestina ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yalikuwa yakijitengenezea yenyewe silaha ndogondogo kwa ajili ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni, lakini hivi sasa wameweza kuingiza kiwango kikubwa cha silaha katika maeneo yao licha ya ulinzi mkali uliowekwa kila kona na utawala wa Kizayuni na sasa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan limezidi kuwakosesha usingizi Wazayuni kama Ukanda wa Ghaza.

Juzi vyombo vya habari vya Palestina viliripoti kuwa, katika kipindi cha saa 24, kulikuwa kumefanyika operesheni 29 dhidi ya wanajeshi vamizi wa Israel na walowezi wa Kizayuni ikiwa ni pamoja na kushambuliwa kwa risasi wanajeshi na walowezi Wazayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *