Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lazima jaribio la waasi wa M23

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetangaza kuwa, limezima jaribio jengine la waasi wa M23 la kuutwaa mji wa Sake ulioko Kivu Kaskazini, wakati mapigano yakiripotiwa kwenye miji mingine ya Rutshuru na Lubero.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mizinga na aina nyingine za kombora zilitumiwa na pande zote mbili, huku jeshi la serikali likivurumisha mabomu kuelekea ngome za waasi kutokea Mugunga kando na kambi za wakimbizi katika mji wa Goma.

Taarifa zinaeleza kuwa makombora yalilenga vijiji vya Vunano pamoja na kilima kinachokaliwa na waasi cha Kihuli kilicho umbali wa kilomita 4 kutokea mji wa Sake.

Barabara inayotoka Sake kuelekea mji wa Mushaki imefungwa kufuatia mashambulizi hayo.

Mwezi Februari mwaka huu pia, jeshi la DRC lilizima jaribio la waasi hao waliokuwa tayari wameukaribia mji wa Sake yapata kilomita 27 kutoka Goma, mashariki mwa taifa hilo.

Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Duru mbalimbali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini zimeripoti kuhusiana na wimbi hilo jipya la wakimbizi.

Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ilialika kikosi hicho cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhika na wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *