Jeshi la Somalia lakomboa mji wa kimkakati kutoka kwa magaidi wa al Shabaab

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuukomboa mji wa kimkakati wa Adanyabal katika eneo la Shabelle ya Kati kutoka kwa magaidi wa al Shabaab.

Rais Mohamud ametangaza habari hiyo wakati akihutubia umma kupitia televisheni ya taifa na huku akigusia tangazo lake la huko nyuma la kuanza vita vya pande zote dhidi ya magaidi wa al Shabab amesema, magaidi hao walikimbia mji huo kabla ya kufika jeshi la Serikali, likisaidiwa na wanamgambo wa koo za eneo hilo.

Katika sehemu moja ya hotuba yake, Rais wa Somalia amesema: “Ni waoga, walikimbia mji bila ya kupigana. Al Shabaab ni historia sasa.”

Vile vile ametumia hotuba yake hiyo kutoa mwito kwa wananchi wa Somalia kuwa kitu kimoja na kuunga mkono mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea dhidi ya genge hilo la kigaidi.

Wakaazi wa eneo hilo Adanyabal wameliambia shirika la habari la Anadolu kwamba magaidi hao waliondoa pampu za maji kutoka kwenye visima viwili vya maji vya mji huo kabla ya kukimbia.

Adanyabal ni mji wa kimkakati ambao umekuwa ngome ya magaidi wa al Shabab tangu 2016 na uko kwenye umbali wa kilomita 245 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.

Vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na wanamgambo wa koo za eneo hilo vimekomboa maeneo makubwa hasa katika jimbo la Hirshabele kutoka kwa genge la al Shabab tangu Rais Mahamud alipotangaza vita vya pande zote dhidi ya magaidi wa al Shabaab.

Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Abdi Barre alisema serikali imeendesha mashambulizi ya pande nyingi dhidi ya wanamgambo wa al Shabaab kijeshi, kifedha, na kiitikadi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *