Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, limewaangamiza wanachama 18 wa kundi la kigaidi la a-Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.
Hayo yameelezwa na Brigedia Jenerali Odowaa Yusuf Rageh Mkuu wa jeshi la Somalia ambaye amebainisha kuwa, magaidi hao wameuawa katikati ya nchi baada ya kutokea mapigano makali kati yao na jeshi.
Aidha amesema kuwa, jeshi la Somalia limefanikiwa kukamata kiwango kikubwa cha silaha sambamba na kuangamiza kikamilifu ngome ya wanamgambo hao katika eneo hilo.
Hayo yanaripotiwa katiika hali ambayo, hivi karibuni Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alitangaza vita dhidi ya kundi la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab ambalo limekuwa likifanya mashambulio na mauaji mara kwa mara katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Tangu mwaka 1992, Somalia haijawahi kuwa na utulivu wa kudumu kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab.
Genge hilo lilianzishwa mwaka 2004 na limejitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida.
Mara kwa mara kundi la kigaidi la al-Shabab limekuwa likishambulia wanajeshi wa serikali na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika hasa katika mji mkuu Mogadishu, kama ambavyo limekuwa likiwashambulia mara kwa mara raia wa Somalia katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Sambamba na machafuko na ukosefu wa amani, Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukame mkubwa unaotishia kuutokkewa baa la njaa.