Vikosi vya jeshi la Syria vimeuzuia msafara wa askari wa jeshi la Marekani kuvuka eneo la kaskazini mashariki ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Syria SANA, msafara huo uliojumuisha magari sita ya kijeshi ya askari vamizi wa Marekani yakiandamana na gari moja la wanamgambo wa Kikurdi wa Syria wa kundi la SDF ulikuwa ukitaka kuingia kijiji cha Salihiyah kilichoko kwenye kiunga cha Qamshali lakini askari wa jeshi la Syria wa kituo cha upekuzi wakauzuia msafara huo na kuulazimisha uondoke katika eneo hilo.
Tukio la jeshi la Syria kuuzuia msafara wa kijeshi wa Marekani lilijiri huku helikopta kadhaa za askari wa jeshi vamizi la Marekani zikiwa zinazunguka katika anga ya eneo hilo.
Katika miezi iliyopita, wananchi wa Syria wamechukua hatua mara kadhaa ya kufunga njia na kuweka uzio wa ngao ya watu huku wakibeba zana za kawaida tu vikiwemo vifaa vya kulimia pamoja na vigongo na virungu na kuizuia misafara ya kijeshi ya askari vamizi wa Marekani kuvuka katika maeneo yao.
Maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na vikosi vamizi vya jeshi la Marekani na wanamgambo wanaoungwa mkono na Washington wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Wakurudi wa Syria SDF katika mkoa wa Al Hasakah na maeneo mengine ya kaskazini ya Syria, kila mara yanashuhudia mikusanyiko ya upinzani ya Wasyria ambao wanapinga hatua zinazochukuliwa na wanajeshi magaidi wa Marekani na wanamgambo wa SDF dhidi ya wakazi wa maeneo hayo.
Serikali ya Syria imeshasisitiza mara kadhaa kuwa wanamgambo hao na wanajeshi vamizi wa Marekani walioko mashariki na kaskazini mashariki ya Syria hawana lengo jengine isipokuwa kupora mafuta ya nchi hiyo na kwamba wanayakalia maeneo hayo kinyume cha sheria.