Jeshi la Yemen likishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi zimeitungua ndege ya pili isiyo na rubani iliyoundwa na Marekani.
Katika miezi kadhaa iliyopita, jeshi la Yemen limefanikiwa kuzitungua droni kadhaa za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia zilizokuwa zikitekeleza operesheni za hujuma katika maeneo mbalimbali ya ardhi ya Yemen.
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree ameeleza katika taarifa kwamba, ndege ya pili ya ujasusi isiyo na rubani iliyoundwa Marekani aina ya ScanEagle imetunguliwa katika anga ya kitongoji cha al Juba kilichoko mkoani Ma’rib.
Yahya Saree ameongeza kuwa, alfajiri ya kuamkia leo, vikosi vya jeshi la Yemen vimeitungua pia kwa kutumia kombora droni nyingine iliyotengenezwa Marekani aina ya MQ-1, iliyokuwa ikitumiwa na kikosi cha anga cha Imarati, katika anga ya mkoa wa al Jawf.
Jeshi la Yemen limesisitiza mara kadhaa kuwa, litaendelea kushambulia taasisi za kistratejia na zana za kijeshi za muungano vamizi wa Saudia, madamu muungano huo wa kijeshi unaendeleza uchokozi wake dhidi ya nchi hiyo. Vikosi vya Sana’a vimetangaza mara kadhaa katika miezi ya karibuni kuwa vimetungua ndege zisizo na rubani za Imarati na Saudia.
Mwezi Machi 2015, Saudi Arabia, ikungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen sambamba na kuiwekea mzingiro wa ardhini, baharini na angani nchi hiyo masikini ya Kiarabu.
Moto wa vita uliowashwa na Saudi na washirika wake dhidi ya Yemen hadi sasa umeshateketeza roho za makumi ya maelfu ya watu, mbali na makumi ya maelfu waliojeruhiwa pamoja na wengine milioni nne waliopoteza makazi yao na kulazimika kuwa wakimbizi…/