Jeshi la Yemen latungua drone ya kijasusi ya Marekani ya ScanEagle huko Ma’rib

Jeshi la Yemen, likishirikiana na wapiganaji wa Kamati za Wananchi, limefanikiwa kutungua ndege isiyo na rubani (drone) ya Kimarekani ya ScanEagle ambayo ilikuwa na jeshi la Saudia kufanya ujasusi katika mkoa wa Ma’rib ambao umekuwa ukishuhudia mapigano makali hivi karibuni.

Msemaji wa Jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree ametangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa, Kitengo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Yemen leo asubuhi kimefanikiwa kutungua drone hiyo iliyokuwa ikitekeleza oparesheni za kiuadui katika wilaya ya al-Jubah mkoani Ma’rib.

Amesema hivi karibuni Jeshi la Yemen litasambaza klipu za namna oparesheni ya kuitungua droni hiyo ilivyotekelezwa.

Mnamo Septemba 27, Jeshi la Yemen likishirikiana na waitifaki wake lilitungua droni nyingine ya kijasusi ya ScanEagel iliyokuwa ikitumiwa na jeshi vamizi la Saudia katika wilaya ya Medghal mkoani Ma’rib.

Wakati huo huo wanamgambo watiifu kwa rais wa zamani wa Yemen Abd Rabbuh Mansour Hadi ambao wamekuwa wakipigana bega kwa bega na wanajeshi vamizi wa Saudia, wamepokea amri ya kuondoa familia zao katika mji wa Ma’rib huku Jeshi la Yemen likikaribia kuchukua udhibiti kamili wa mkoa huo wa kistratijia.

Ikumbukwe kuwa, Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Makumi ya maelefu ya watu wa Yemen, hasa wanawake na watoto wamepoteza maisha moja kwa moja kutokana na vita hivyo huku malaki au hata mamilioni ya wengine wakipoteza maisha kutokana na maafa na majanga yaliyosababishwa na vita hivyo. Watoto Wayemen ndio waathirika wakuu kwani wengi wamekosa lishe, dawa na matibabu kutokana na vita hivyo vya Saudia dhidi ya nchi yao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *