Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema kuwa, mkoa wa al Jawf wa nchi hiyo umeshakombolewa kikamilifu kilichobakia ni mabaki ya hapa na pale tu ya wavamizi na mamluki wao.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema hayo na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Yemen vimeendesha operesheni ya Fajr al Swahra (Mapambazuko ya Jangwani) na kufanikiwa kukomboa maeneo yaliyokuwa yamebakia ya mkoa wa al Jawf.
Amesema, katika operesheni ya Mapambazuko ya Jangwani, majeshi ya Yemen yamefanikiwa kuwazidi nguvu na kuwafurusha mamluki wa madola vamizi na kukomboa maeneo mengi makubwa kiupana na kiurefu. Amesema operesheni hiyo imefanikiwa kukomboa kilomita mraba 200 za maeneo yaliyokuwa yanakaliwa kwa mabavu na wavamizi wanaoongozwa na Saudi Arabia.
Ameongeza kuwa, mkoa wa al Jawf umeshakombolewa kikamilifu isipokuwa baadhi ya maeneo ya jangwani na kusisitiza kuwa, operesheni ya Mapambazuko ya Jangwani imemsababishia hasara kubwa adui na idadi kuwa ya silaha zimechukuliwa ngawira.
Msemaji huyo wa majeshi ya Yemen vile vile amesema, tunajibu mashambulizi kwa mashambulizi na hatutetereki wala kurudi nyuma hata kidogo katika kupigania haki yetu ya kisheria ya kulihifadhi na kulikomboa taifa letu.
Brigedia Jenerali Yahya Saree amefafanua pia kwamba hivi sasa majeshi ya Yemen yameingia kwenye awamu mpya ya kupambana na njama za muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na ametoa mwito kwa wananchi wote wa Yemen kushiriki katika vita vya ukombozi na kupigania uhuru wa nchi yao.
Amesema, vikosi vya Yemen vitajibu jinai zote zinazofanywa na madola vamizi na kwamba wananchi wanamuqawama wa Yemen wana njia nyingi za kulipiza kisasi jinai na ukatili wanaofanyiwa.