Jeshi laangamiza makumi ya magaidi wa kundi la Ash-Shabab katikati ya Somalia

FARAAN: Mashuhuda na maafisa wa serikali katika eneo hilo wamesema, mapigano yalianza wakati wanachama wa kundi la kigaidi la Ash-Shabab walipokivamia kitongoji cha Bahdo kilichoko kilomita 60 mashariki ya mji huo wa Adado.

Msemaji wa jeshi la Somalia Yabal Haji Aden ameviambia vyombo vya habari kuwa wanamgambo wa Ash-Shabab walianzisha shambulio lao kwa kuripua gari lililosheheni mada za miripuko karibu na sehemu ya kuingilia kitongoji hicho na kusababisha mapigano makali ya mitaani baina yao na wanamgambo wa kujitolea wa kitongoji hicho wakisaidiwa na vikosi vya jeshi.

Gavana wa mkoa wa Galguduud Ali Elmi Ganey amesema, vikosi vya serikali vimeua wanamgambo wapatao 47 wa kundi la kigaidi na lenye misimamo ya kufurutu ada la Ash-Shabab.

“Magaidi wameyaonja mauti, ndani na nje ya mji. Wameacha maiti 47, bunduki na zana za kijeshi”, amesema Elmi Ganey.

Wakazi na maafisa wa eneo hilo wamesema, watoto watatu, alimu mashuhuri wa kidini na askari watatu waliuawa pia wakati wa mapigano hayo…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *