Jibu la Iran kwa taarifa ya pamoja ya China na Saudia na madai yaliyoibuliwa

Mohammad Jamshidi, Mkuu wa masuala ya kisiasa katika Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter kujibu matamshi ya Rais wa China aliyotoa wakati wa ziara yake nchini Saudi Arabia.

Jamshidi ameandika: “Wenzetu Wachina inapasa wakumbuke kuwa wakati Aal Saud na Marekani zilipoyaunga mkono makundi ya kigaidi ya DAESH (ISIS) na Al-Qaeda huko Syria na kuiteketeza Yemen kupitia uvamizi wa kinyama wa kijeshi, ni Iran ndio iliyopigana vita na magaidi mpaka amani na uthabiti vikapatikana na kuzuia ugaidi usisambae kuelekea Mashariki na Magharibi”.

Inafaa kuashiria hapa kuwa baada ya mikutano aliyofanya Rais Xi Jinping wa China na viongozi wakuu wa Saudi Arabia, siku ya Ijumaa China na Saudia zilitoa taarifa ya pamoja, ambayo katika sehemu yake moja yaliashiriwa madai dhidi ya Iran na matakwa kadhaa pia ya kutaka Tehran iyatekeleze. Katika taarifa yao hiyo ya pamoja, -na bila kuashiria chochote kuhusu uafriti wa Magharibi wa kukwamisha kufufuliwa kwa mapatano ya nyuklia JCPOA-, China na Saudia zimesisitiza juu ya ulazima wa kuimarishwa mashirikiano ya pamoja kati ya Beijing na Riyadh ili kupata hakikisho kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani. Pande hizo mbili pia zimeitaka Iran itoe ushirikiano kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA na kuheshimu Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia NPT. Katika sehemu nyingine ya taarifa yao, China na Saudi Arabia zimetilia mkazo umuhimu wa Iran kuheshimu misingi ya ujirani mwema na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi zingine.

Pamoja na hayo, yaliyosemwa na kunenwa na Riyadh na Beijing hayakuishia kwenye taarifa ya pamoja tu ya pande hizo mbili, kwani baada ya kutolewa taarifa hiyo, rais wa China alitia saini taarifa nyingne katika kikao cha pamoja na viongozi wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi GCC, ambayo iliikosoa na kuilaumu Iran. Ndani ya taarifa hiyo imesisitizwa kuwa, uhusiano kati ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na Iran inapasa ufuate misingi ya ujirani mwema na kutoingilia masuala ya upande wa pili, kuheshimu uhuru, mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi za nchi zote, kusuluhisha mizozo kwa njia za amani na kulingana na Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa bila kutumia nguvu au vitisho pamoja na kudumisha usalama na uthabiti wa kikanda na kimataifa.

Madai hayo yametolewa katika hali ambayo, ukweli usioweza kukanushika uko kinyume chake. Kwanza ni kwamba, kama ulivyokiri Wakala wenyewe wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na ripoti zake mbalimbali, shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani hazijaonyesha mkengeuko wowote wa kuelekea kwenye malengo ya kijeshi. Suala hili limesisitizwa tena hivi karibuni na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo wa IAEA. Isitoshe, siku chache zilizopita, Mkurugenzi wa Intelijensia ya Taifa ya Marekani, Avril Haines alitangaza kinagaubaga kuwa, hakuna taarifa zozote zinazoonyesha kwamba Iran imechukua uamuzi wa kuunda silaha za nyuklia.

Maelezo yote haya yanaonyesha kuwa, kinyume na madai yaliyotolewa katika taarifa ya Beijing na Riyadh, kimsingi ni kwamba Tehran haina nia ya kuuelekeza mpango wake wa nyuklia kwenye malengo ya kijeshi hata ihitajike dhamana ya kuhakikisha kuwa unafanyika kwa malengo ya amani. Isitoshe, China yenyewe, ambayo ni mmoja wa wanachama wa kundi la 4+1, kabla ya kauli yake ya sasa, imekuwa ikieleza kila mara kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani na kuuunga mkono mpango huo.

Suala jingine muhimu lililoashiriwa katika taarifa ya pamoja ya China na Saudi Arabia ni kuishutumu Iran kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba inaingilia masuala ya ndani ya majirani zake na kwa namna fulani kutokuwa na sera ya ujirani mwema. Suala hili kimsingi sio sahihi. Ukweli ni kwamba, Saudi Arabia, pamoja na baadhi ya nchi nyingine za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, baada ya kuanza machafuko nchini Syria mwaka 2011, ziliutumia muungano wa nchi za Magharibi na za Kiarabu pamoja na Uturuki, kuyazatiti kwa zana za kijeshi na silaha makudi mbalimbali ya kigaidi nchini Syria, na  kuwatwisha watu wa nchi hiyo vita vya muda mrefu, japokuwa vita hivyo vimegonga mwamba na havijafikia lengo lake ovu.
Lakini mkabala wake, Iran- na kama alivyoashiria mkuu wa masuala ya kisiasa wa Ofisi ya Rais- ikiwa bega kwa bega na waitifaki wake, ilipambana kwa nguvu zote katika ardhi za Syria na Iraq na kuushinda ugaidi unaoungwa mkono na Wasaudi na tawala zingine za Kiarabu zenye fikra mgando. Utawala wa Saudi Arabia ukishirikiana na Muungano wa Falme za Kiarabu, zilianzisha vita pia vya umwagaji damu dhidi ya Yemen kuanzia Machi 2015 na kuua na kujeruhi makumi ya maelfu ya raia, mbali na kuteketekeza miundombinu ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu, suala linaloonyesha wazi kwamba sera ya Riyadh ni ya kushupalia vita na kuingilia masuala ya kikanda. Masuala yote hayo yanaonesha kuwa, hatua za Iran, iwe ni kuhusiana na mpango wake wa nyuklia au sera zake za kieneo, zinafuata mkondo sahihi na wa kimantiki; na madai yaliyotolewa dhidi ya Tehran hayana msingi wowote.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *