Msemaji wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amesema kuwa, harakati hiyo itaendeleza mapambano yake katika mwaka huu mpya wa 2023 hadi itakapokomboa kila shibri ya ardhi za Palestina na haitetereshwi hata kidogo na serikali mpya ya kifashisti na yenye misimamo mikali kupindukia ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hayo yameripotiwa na tovuti ya habari ya al ‘Ahd ambayo imemnukuu Tariq Salmi akisema hayo jana (Jumapili) na kuongeza kuwa, tumemaliza mwaka wa 2022 ambao umeshuhudia muqawama wa kishujaa na wa kupigiwa mfano wa wananchi wa Palestina, tumeshuhudia kujitolea muhanga mno wananchi wa Palestina katika vita dhidi ya utawala wa Kizayuni na hatukusita hata mara moja kuendesha mapambano dhidi ya wavamizi wa Quds.
Amesema, katika mwaka huu mpya wa 2023 pia, tutaendeleza mapambano yetu katika maeneo yote ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yakiwemo ya Jenin, Quds na Nablos kwa mori na nguvu zile zile na makamanda wetu waliouawa shahdi kama shahid Taisir al Jaafari na Khalid Mansour hadi tutakapokomboa ardhi zote za Palestina.
Msemaji huyo wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina pia amesema, serikali ya kifashisti, ya mrengo wa kulia na yenye misimamo mikali kupindukia ya Benjamin Netanyahu haiwezi kuitia woga wala kuiteteresha Jihad al Islami.
Naye Ziyad al Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadi al Islami ya Palestina amesema, mwaka mpya wa 2023 umesheheni changamoto na mapambano na sisi hatuna chaguo jingine isipokuwa kushadidisha mapambano dhidi ya Wazayuni.
Amesema, mwaka ulioisha wa 2022 ulikuwa mwaka wa kutotetereka na wa kusimama imara taifa la Palestina katika mapambano dhidi ya Wazayuni, na mwaka huu pia wa 2023 utaendelea kuwa wa mshikamano baina ya makundi ya muqawama ya Palestina na kuendeleza intifadha ya silaha kama tunavyoona leo katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi.