Ijumaa alasiri, jeshil la utawala wa kigaidi wa Israel lilitekeleza jinai kubwa dhidi ya Wapalestina kupitia mashambulizi yaliyopewa jina la “Operesheni ya Alfajiri”, katika maeneo yanayodhibitiwa na harakati ya Palestina ya Jihad Islami katika Ukanda wa Gaza.
Katika jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni, Wapalestina 12 akiwemo mtoto wa miaka 5, pamoja na Taysir al-Jabari, kamanda wa eneo la kaskazini katika Brigedi ya Quds, waliuawa shahidi. Katika mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni, maeneo ya kundi la Jihad Islami la Palestina na wanachama wake walilengwa. Al-Ja’bari, ambaye alichaguliwa kama mrithi wa Shahidi Baha Abul Ata mnamo mwaka 2019, alinusurika majaribio mawili ya mauaji mnamo 2012 na 2014. Al-Jabari alikuwa kamanda wa eneo la kaskazini la Brigedi ya al-Quds katika operesheni ya “Upanga wa al-Quds” mwaka 2021 na alikuwa miongoni mwa wasimamizi wa uundaji wa makombora ya harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu, ukiwemo mfumo wa makombora wa Jihad al-Islami uliozinduliwa mwezi Mei 2021.
Kwa kumuua al-Jabari, utawala huo wa Kizayuni umetaka kulipiza kisasi cha oparesheni ya mwaka uliopita ya Upanga wa al-Quds na wakati huo huo kumfuta mmoja wa makamanda muhimu wa Jihad Islami. Mbali na al-Jabari, utawala wa Kizayuni umewatia mbaroni makumi ya wanachama wa harakati hiyo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Gazeti la Kizayuni la Maariv limedai kuwa, Wapalestina hao walihusika katika operesheni tofauti dhidi ya utawala wa Israel.
Hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni imekosolewa hata ndani ya utawala huo wenyewe. Gal Berger, mchambuzi wa Israel ameitaja hatua hiyo kuwa ni kosa kubwa na kuandika: “Sasa makundi yote ya Wapalestina yanatulenga sisi kwa jina la Jihad Islami, na yote yameungana dhidi yetu, ambapo msababishaji pekee wa hali hii ni Yair Lapid Waziri Mkuu wa Israeli.”
Katika kukabiliana na jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni, makundi ya mapambano ya Palestina yamesisitiza katika taarifa kwamba, mapambano na umoja wao ndio utakaosalia kuwa ncha ya mshale dhidi ya jinai za utawala huo ghasibu huku yakisisitiza kuwa jinai hiyo haitapita bila kupatiwa jibu. Kuhusiana na suala hilo makundi ya mapambano ya Palestina bila kupoteza wakati yamejibu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza kupitia mashambulizi ya makombora kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu, makombora ambayo aghlabu yalishindwa kutunguliwa na mfumo wa ulinzi wa utawala wa Kizayuni.
Kufuatia jibu madhubuti la makundi ya mapambano ya Palestina, Tor Vansland, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Asia Magharibi, ametaka kusimamishwa mara moja majibu ya makombora ya makundi hayo dhidi ya jinai za utawala wa kigaidi wa Isreal. Huku akipuuza mauaji ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni, Vansland amesema katika taarifa yake: “Kuongezeka mvutano katika Ukanda wa Gaza ni hatari kubwa, Urushaji wa makombora kutoka Gaza lazima usitishwe mara moja, na ninatoa wito kwa pande zote kujiepusha kuongeza mvutano.”
Duru zingine pia zinaeleza kuwa utawala wa Kizayuni umeomba usuluhishi ili kumaliza mzozo huo, lakini makundi ya mapambano ya Palestina yamekataa ombi hilo. Upinzani wa Jihad Islami dhidi ya upatanishi unatokana na sababu kwamba inaamini kuwa zama za utawala wa kibaguzi wa Israel kushambulia Wapalestina na kukimbia zimekwisha na kuwa makundi ya Wapalestina yana haki ya kutoa jibu la kisawa sawa kwa jinai za utawala huo.
Nukta ya mwisho ni kwamba mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya ya Jihad Islami ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza yametekelezwa kwa mara nyingine tena huku mwenendo wa uchaguzi wa utawala huo ukikabiliwa na mkwamo wa kisiasa. Vita vya siku 12 vya mwaka jana pia vilitokea baada ya waziri mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu kushindwa kuunda baraza la mawaziri. Sasa baraza la mawaziri la muungano wa Lapid na Bennett limeporomoka na uchaguzi mwingine wa bunge umepangwa kufanyika Novemba ijayo.