Kamati ya Palestina katika Bunge la Jordan imesisitiza kuwa, Waislamu wana mamlaka mutlaki kwa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa ulioko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kamati hiyo imeuonya utawala ghasibu wa Israel na kuutaka usiitahini subira ya Waislamu bilioni 2 ulimwenguni. Msimamo huo wa Kamati ya Palestina katika Bunge la Jordan umetolewa kufuatia matamshi ya Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa Israel ambaye amezungumzia mamlaka ulionayo utawala huo kwa msikiti wa al-Aqswa.
Kamati hiyo imelaani vikali matamshi hayo na kuitahadharisha Israel kwa kuiambia kwamba, isitahini subira ya Waislamu bilioni 2 duniani. Akisoma taarifa hiyo, Muhammad al-Zahrawi, Mkuu wa Kamati ya Palestina katika Bunge la Jordan amezungumzia matokeo mabaya ya kuendelea uvamizi wa Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqswa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kueleza kwamba, Israel ni nguvu ya uvamizi wa kikoloni ambayo imekuwa ikifanya ugaidi na kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Palestina.
Wakati ulimwengu ukiendelea kulaani hatua zisizo za kibinadamu za Israel huko Palestina, Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu ametangaza kijeuri kabisa kwamba, utawala huo haujali chochote na kwamba, utachukua maamuzi yote yanayohusiana na msikiti wa al-Aqswa pamoja na mji wa Baytul-Muqaddas kwani ndio wenye mamlaka na maeneo hayo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni umepanga kupitisha mpango wa kujenga nyumba mpya zipatazo elfu nne katika eneo la Ufukwe wa Magharibi, Palestina inayokaliwa kwa mabavu, tangazo ambalo limeendelea kulalamikiwa kieneo na kimataifa.