Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeanza kuchukua hatua kwa lengo la kutokomeza silaha za atomiki za utawala haramu wa Israel baada ya nchi 149 wanachama wa umoja huo kuunga mkono azimio linaloutaka utawala huo wa Kizayuni “uache kufuatilia uzalishaji, uundaji, majaribio au kutaka kuwa na silaha za nyuklia” na “kuachana na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia”.
Azimio hilo ambalo hutolewa kila mwaka kwa lengo la kuzuia uenezaji silaha za nyuklia, awali liliwasilishwa na Misri kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuungwa mkono na Mamlaka ya Ndani ya Palestina pamoja na nchi 19 zikiwemo Bahrain, Jordan, Morocco na Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE). Azimio hilo linaeleza kwamba, utawala wa Kizayuni ndio pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati na ni miongoni mwa nchi chache kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa ambayo haijatia saini Mkataba wa NPT.
Wakati wa mjadala kuhusu kifungu kinachohusu “uwezo wa kinyuklia wa Israel”, mwakilishi huyo wa Kuwait katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna alisema, kuna ulazima wa uwezo wa kinyuklia wa utawala huo kuchunguzwa katika vyombo vya upangaji sera za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Lakini kwa kuzingatia kuwa maazimio ya Baraza Kuu ni ya utoaji ushauri na mwongozo, baraza hilo linaweza kutumia utaratibu ujulikanao kama “muungano kwa ajili ya amani” ili kuyafanya maazimio linayopitisha yaweze kutekelezeka.