Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao mara mbili asubuhi na jioni kujadili matukio mapya yanayojiri Palestina.
Hata kama kikao hicho hakikufikia mwafaka unaoeleweka, lakini kilitoa fursa kwa nchi mbalimbali kubainisha mitazamo yao, ambayo kwa ujumla imedhihirisha jinsi utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unavyokiuka misingi na sheria za kimataifa pamoja na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Saeed Iravani, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, yeye ameeleza katika hotuba kwamba kulingana na ripoti mbalimbali, tangu mwaka 2006 hadi sasa, mwaka huu 2022 ndio ulioshuhudia vifo vingi zaidi vya Wapalestina waliouliwa shahidi na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel; na kwa sababu hiyo, akatilia mkazo ulazima wa Baraza la Usalama kuwahami na kuwasaidia watu wa Palestina.
Abdulaziz ameashiria pia unafiki wa utawala wa Kizayuni na akaeleza kwamba: hakuna mantiki yoyote kwa Israel kujitafutia umaarufu kwa kulaani uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine, ilhali yenyewe imeivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya nchi ya Palestina katika hatua inayokinzana na azimio nambari 181 la mwaka 1947 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo limeeleza bayana kuhusu uundwaji wa nchi mbili.
Sio tu Israel haiko tayari kukaa kwenye meza ya mazungumzo ya ana kwa ana kujadili uundwaji wa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baitul Muqaddas (Jerusalem), lakini inafanya kila njia pia ili kuhakikisha inauhodhi kikamilifu mji huo na wakati huohuo inafanya mauaji na kila aina jinai ndani ya Quds kwenyewe na maeneo mengine ya ardhi ya Palestina inayoikalia kwa mabavu, ambao ni ukiukaji wa wazi kabisa wa maazimio ya miaka na miaka yaliyopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; lakini ajabu ni kwamba haihojiwi wala kuulizwa chochote kwa lolote inalofanya.
Kusema kweli Palestina imekuwa mithili ya kapu la kumiminia makumi kwa makumi ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu la umoja huo ambayo yamepitishwa ili kulinda angalau haki chache za Wapalestina na vilevile misingi na sheria za kimataifa ambazo zimewekwa kwa ajili ya kuwaadhibu wanaovamia na kukalia ardhi za wengine kwa mabavu, kuweka vizuizi dhidi ya hatua zao hizo na pia kutetea na kulinda haki za mataifa yaliyovamiwa na kukaliwa kijeshi. Laiti kama maazimio yote hayo, -ambayo yameeleza bayana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuhusu ulazima wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuondoka bila masharti yoyote katika ardhi ulizozivamia na kuzikalia kwa mabavu mwaka 1967 ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza huko Palestina na Miinuko ya Golan ya Syria na ambayo yamebainisha na kusisitiza juu ya kutobadilishwa muundo wa kijiografia na wa idadi ya watu wa maeneo hayo- yangekuwa yametekelezwa hadi sasa; na au kama haki ya Kujilinda Kisheria iliyoelezwa wazi katika Hati ya Umoja wa Mataifa ingetambuliwa rasmi kwa ajili ya Wapalestina na si kupinduliwa maana yake kwa misamiati mingine kama utumiaji nguvu na ugaidi, mgogoro wa Palestina usingerefuka na kufikia hapa ulipofika na wala Wazayuni wasingepata fursa ya kuutumia vibaya na kwa maslahi yao kwa kiwango hiki tunachoshuhudia.
Ukweli wa mambo ni kuwa miamala hiyo ya kibaguzi na upendeleo ndiyo iliyorefusha mgogoro wa Palestina na kuendelea uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Wazayuni kupitia ujenzi wa vitongoji; na kwa muktadha huo, wanaobeba dhima kuu ya ukandamizaji, ukaliaji ardhi na jinai zinazofanywa na Wazayuni katika ardhi za Palestina ni watu waliopelekea kuwepo ubaguzi na upendelezo huo, ambao si wengine isipokuwa nchi za Magharibi na hasa Marekani. Lakini sambamba na hao hatuwezi kufumbia jicho pia uzembe na kutowajibika kwa Umoja wa Mataifa. Katika faili la utendaji wa Umoja wa Mataifa watu kama hayati Kofi Annan, walijitahidi kuhakikisha utendaji wa umoja huo unakaribiana na malengo na majukumu uliyoainishiwa, lakini kwa masikitiko ni kwamba katika miongo ya karibuni, watu waliokabidhiwa jukumu la kuongoza Umoja wa Mataifa wameiweka mbali taasisi hiyo kuu ya kimataifa na malengo yake na badala yake kuifanya iende sambamba zaidi na siasa na sera za madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, jambo ambalo limeupatia fursa zaidi utawala haramu wa Kizayuni ya kufanikisha malengo na maslahi yake.
Kwa msingi huo, hatua inayopasa kuchukuliwa ili Umoja wa Mataifa uweze kutekeleza majukumu na malengo uliyoainishiwa ni kufanyika mageuzi ya kimuundo katika asasi hiyo, jambo ambalo kwa bahati mbaya, hadi sasa halijafanikiwa. Ama kwa upande wa yanayohusiana na Palestina, japokuwa Serikali ya Mamlaka yake ya Ndani ingali imeweka tamaa kwa Umoja wa Mataifa na taasisi zingine zenye mfungamano nao na hivyo kila baada ya muda kuzielekea taasisi hizo, lakini wananchi wa Palestina, kama inavyoshuhudiwa wakati huu huko Jenin na Nablus na kuenea katika maeneo mengine ya Ukingo wa Magharibi, wamefikia hitimisho kwamba, njia ya uwokozi na ya kukabiliana na utawala katili wa Kizayuni ili usilikalie tena eneo la Ukingo wa Magharibi ni Muqawama wa mtuutu wa bunduki; na katika kufanikisha lengo hilo wanayaunga mkono makundi mapya ya mapambano likiwemo la ‘Arinul-Usud, yaani Pango la Simba na wala hawajipi matumaini tena ya kupata msaada kwa Umoja wa Mataifa au hata kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.