Makumi ya asasi za Palestina na za kimataifa zimeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ifanye uchunguzi kuhusu jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na Falastin al-Yaum, jumuiya 198 za Palestina na za kimataifa zimemtaka Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na Silvia Fernández de Gurmendi, Hakimu wa mahakama hiyo kuchunguza jinai za kivita za utawala wa Kizayuni dhidi ya asasi za kiraia na wananchi wa Palestina kwa ujumla.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika risala yao kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, taasisi hizo zimetaka kulaaniwa hadharani hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuziweka asasi za kiraia za Palestina kwenye orodha ya ugaidi na pia kuilazimisha Israel ibadilishe uamuzi wake huo.
Taasisi hizi pia zimetaka jinai zilizofanywa na Israel wakati wa shambulio lake la kijeshi lisilo na uhalali ililofanya dhidi ya Ukanda wa Gaza Septemba 2022 zijumuishwe katika uchunguzi unaoendelea kufanywa kuhusu hali ya Palestina.
Katika waraka wa jumuiya hizo, umetiliwa mkazo pia ulazima wa kuharakishwa uchunguzi kuhusu hali ya Palestina na kubainishwa kwamba jinai zote zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina, ikiwa ni pamoja na kuzikandamiza taasisi za Palestina ni hatua zisizo za kibinadamu na miongoni mwa jinai za ubaguzi wa rangi dhidi ya binadamu na zinapasa kuchunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Jumuiya hizo 198 za Palestina na za kimataifa vilevile zimetaka zichukuliwe hatua mwafaka kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ili kuzuia vitendo vya kibaguzi na hatua za wanajeshi wa Kizayuni za kufanya jinai zaidi za kivita na zinazokinzana na ubinadamu dhidi ya wananchi wa Palestina.
Ikumbukwe kuwa wakati utawala wa Kizayuni unafanya mashambulizi ya kinyama kila siku katika maeneo ya Palestina huku watoto wa Kipalestina wakiwa waathirika wakubwa na wahanga wa mashambulizi hayo, serikali za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu zinafumbia macho jinai hizo kama kwamba hakuna ukiukaji wowote wa haki za binadamu unaofanywa na Israel.