Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) yasisitiza wasichana kupatiwa elimu Afghanistan

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ametoa wito wa kufanyika kampeni ya kuandaa mazingira ya kupatiwa elimu wasichana wa Afghanistan.

Wiki iliyopita, serikali ya Taliban ilitoa taarifa ya kupiga marufuku wasichana kuendelea na masomo katika vyuo vikuu vya nchi hiyo. Hatua hiyo imekabiliwa na malalamiko mengi ndani na nje ya Afghanistan. Kabla ya hapo Taliban ilikuwa imewapiga marufuku kuendelea na masomo wasichana wa darasa la sita na kuendelea.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sauti ya Afghanistan (Ava), Hossein Ibrahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ameeleza katika taarifa kwamba: “hakuna hoja yoyote katika mtazamo wa sharia za Kiislamu ya kuwapiga marufuku wasichana kwenda vyuo vikuu na mashuleni.”
Katibu Mkuu wa OIC ameongezea kwa kusema: uamuzi wa serikali ya Taliban wa kuwapiga marufuku wanawake kupata elimu ya mashuleni na vyuo vikuu kwa kisingizio kuwa jambo hilo linakinzana na sharia za Kiislamu haukubaliki.
Hapo awali, Shekhe Ahmed Al-Tayeb, Shekhe Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha Misri na Mkuu wa Baraza la Wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu, alieleza kwamba hatua ya Taliban ya kuwapiga marufuku wanawake na wasichana kupata elimu haina mantiki na akalitaka kundi hilo litafakari upya uamuzi wake huo.
Kuhusiana na suala hilo, Farhad Abrar, mhadhiri wa chuo kikuu, anasema: kupinga kufunguliwa tena skuli na vyuo vikuu kwa ajili ya wasichana wa Afghanistan kutapanua mpasuko uliopo kati ya watu wa Afghanistan na Taliban.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *