Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu yasisitiza kuunga mkono haki za Wapalestina

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imesisitiza kuendelea kutetea na kuuunga mkono haki za wananchi madhulumu wa Palestina.

Taarifa ya OIC iliyotolewa leo kwa mnasaba wa kutimia miaka 105 tangu kutolewa  Azimio la Balfour imesisitiza kuwa, jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono mapambano ya kiadilifu ya wananchi wa Palestina yenye lengo la kupigania haki zao za kitaifa.

Sambamba na sisitizo hilo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitaka jamii ya kimataifa  kufanya juhudi maradufu za kubadilisha dhulma hii ya kihistoria sambamba na kuchukua hatua za maana kwa ajili ya kuhitimisha uvamizi wa utawala haramu wa Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Sehemu nyingine yya taarifa hiyo ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitaka jamii ya kimataifa kupigania kwa nguvu zote haki za Wapalestina ikiwemo haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao za asili.

Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo miaka 105 iliyopita  lilitolewa Azimio la Balfour. Tangazo hilo lililotolewa na Arthur James Balfour Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa wakati huo wa Uingereza liliandaa uwanja wa kuasisiwa utawala haramu wa Israel huko katika ardhi za Palestina zilizokuwa chini ya wakoloni wa Uingereza.

Tangazo hilo pia liliipa idhini serikali ya London kuunda utawala wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina sanjari na kuitaka serikali hiyo kufanya kila iwezalo kufanikisha jambo hilo.

Mwishowe miaka 30 baada ya kutolewa tangazo hilo la kikoloni mnamo mwaka 1948, utawala wa Kizayuni ulianzishwa kwa msaada wa Uingereza na Marekani na kwa kukanyagwa haki zote za wananchi wa Palestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *