Maafisa usalama nchini Kenya wametumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kukabiliana na wafuasi wa kinara wa upinzani nchini humo Raila Odinga, ambao wamejitokeza kwa wingi kushiriki maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.
Vikosi vya polisi wa kutuliza ghasia nchini Kenya vimeingia mitaani kukabiliana na maandamano hayo yaliyoitishwa na Odinga kulalamikia kupanda kwa gharama za maisha nchini humo, licha ya maandamano hayo kupigwa marufuku.
Odinga alisema ameitisha maandamano hayo kupinga ongezeko la gharama za maisha, kiwango kikubwa cha ushuru wanaotozwa Wakenya, na uchaguzi “ulioibiwa” wa Agosti mwaka uliopita 2022.
Katika kitongoji cha makazi duni ya Kibera jijini Nairobi, waandamanaji walichoma matairi huku vijana kadhaa wakikamatwa katika moja ya maeneo ya maandamano katika mji mkuu wa Nairobi. Baadhi ya waandamanaji wamesikika wakipiga nara za “Ruto lazima aondoke”.
Odinga ambaye alishindwa katika uchaguzi wa Rais, Agosti 2022 dhidi ya William Ruto, ameapa kwamba maandamano hayo yataendelea kila siku ya Jumatatu. Watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye maandamano hayo, mbali na mamia ya watu wakiwemo viongozi wa ngazi za juu wa muungano wa Azimio la Umoja kutiwa mbaroni kwa kushiriki maandamano hayo.
Maandamano haya yamefanyika licha ya Mkuu wa polisi wa Kaunti ya Nairobi, Adamson Bungei kusema jana Jumapili kwamba, maandamano hayo si halali kwa kuwa polisi walipokea maombi ya kufanya maandamano mawili mwishoni mwa Jumamosi na mapema Jumapili wakati kwa kawaida taarifa ya mkutano wa hadhara inatakiwa kutolewa siku tatu kabla.
Huko nchini Afrika Kusini, polisi imesema kuwa imewatia nguvuni watu 87 wakiwemo viongozi na wanasiasa nchini humo kuhusiana na maandamano ya upinzani.
Waziri wa Polisi nchini humo, Bheki Cele amesema miongoni mwa waliokamatwa leo Jumatatu walikuwa ni kutoka jimbo la Gauteng. “Wengi walipatikana wakitengeneza vilipuzi vya moto, wakifunga barabara na kujaribu kuwazuia watu kwenda kazini. Hawakuandamana kwa amani ,” alisema.
Aliongeza kuwa zaidi ya magurudumu 24,000 yalikamatwa na polisi katika miji tofauti. Cele Alisema kuwa polisi wanashirikiana na wanajeshi kuimarisha hali ya utulivu.
Chama kikuu cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinaongoza kile knachoitwa ‘’kufungwa kwa shughuli za kitaifa’’. Kilianza maandamano hayo jana Jumapili saa sita usiku. EFF kinatoa wito wa kujiuzulu kwa Rais Cyril Ramaphosa na kumalizika kwa mzozo wa nishati nchini humo.
Nchi nyingine za Afrika zilizoshuhudia maandamano hii leo Jumatatu ya Machi 20 kwa sababu tofauti ni Nigeria, Senegal, Gambia na Tunisia.