Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri ametoa onyo kali na kusema ushirikiano wa jeshi la kigaidi la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na waitifaki wao waliowapa vituo vya kijeshi ni tishio kwa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika ujumbe, Meja Jenerali Baqeri amesema kamandi ya jeshi la kigaidi la Marekani ijulikanayo kama CENTCOM, ambayo inaendesha oparesheni zake Asia Magharibi, kusini na kati, katika miezi ya hivi karibuni imeondoa manowari zake za kivita katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman lakini inafidia hatua hiyo kwa kuujumuisha katika CENTCOM utawala haramu wa Israel ambao ni maarufu kwa kuua watoto.
Meja Jenerali Baqeri amesema kwa mtazamo wa Iran, uwezo wa kijasusi na hata wa kioparesheni wa Marekani na waitifaki wake sasa umekabidhiwa utawala ghasibu wa Israel jambo ambalo sasa ni tishio linaloongezeka dhidi ya Iran.
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran amesema kuhusiana na kadhia hiyo, Iran imetuma ujumbe na kutoa onyo la maandishi kwa nchi ambazo zina vituo vya kijeshi vya Marekani. Aidha amesema mbali na hayo katika kujibu tishio hilo jipya majeshi ya Iran yametoa onyo kwa maadui kupitia kuimarisha doria angani na baharini na pia wigo wa kupokea taarifa za siri sambamba na kukithirisha mazoezi mabali mbali ya kijeshi yakiwemo ya baharini, makombora na ndege zisizo na rubaini.
Meja Jenerali Baqeri amesisitiza kuwa, ushauri wa daima na wa kirafiki wa Iran kwa nchi jirani ni kuwa, udugu na ushirikiano kwa ajili ya kudumisha usalama katika eneo unapaswa kutuekelezwa bila kutegemea madola ajinabi.