Kanada na Uingereza zilishirikiana kusafirisha wasichana kujiunga na magaidi wa Daesh

Idara ya ujasusi ya Kanada ilihusika katika kutuma wasichana kwenda kujiunga na kundi la kigaidi la Daesh au ISIS na serikali ya Uingereza ilijua nafasi ya Kanada katika kashfaa hiyo lakini ikajizuia kuifichua.

Hayo yamefichuliwa na mwandishi ambaye anaeleza kuhusu kisa cha Shamima Begum, raia wa zamani wa Uingereza ambaye alijiunga na ISIS mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 15.

Mwaka jana, serikali ya Uingereza ilifuta uraia wake wa Uingereza alipokwenda Syria kujiunga na ISIS; Lakini sasa imebainika kuwa aliingizwa nchini Syria kinyemela na mtu aliyekuwa akifanya kazi katika idara ya ujasusi ya Kanada, na kwamba Uingereza ilifunika kwa makusudi nafasi hiyo ya Canada.

The Secret History of the Five Eyes: The Untold Story of the Shadowy International Spy Network ni kitabu kilichoandikwa na Richard Kerbage, ripota wa zamani wa masuala ya usalama na upepelezi wa gazeti la Sunday Times, ambaye alifanya uchunguzi wa kina kuhusu mashirika ya kijasusi ya Australia, Kanada, New Zealand, Uingereza na Marekani.

Kanada pia ilifahamu kuwa jasusi aliyehusika katika kusafirisha wasichana wajiunge na ISIS alikuwa pia jasusi wa pande mbili ambaye alikuwa akihudumu kama jasusi wa ISIS na pia jasusi wa Shirika la Ujasusi la Kanada (CSIS).

Mara tu baada ya kukamatwa jasusi huyo nchini Uturuki, Canada iliifahamisha Uingereza kwa siri kuhusu kadhia hiyo na ikataka habari za kuhusika Kanada zisifichuliwe.

Msemaji wa Huduma ya Ujasusi ya Usalama wa Kanada amesema hawezi kuthibitisha au kukanusha hadharani maelezo ya uchunguzi huo.

Msemaji wa serikali ya Uingereza pia amedai: Ni sera yetu ya muda mrefu kutotoa maoni juu ya masuala ya kijasusi.

Shamima Begum, mwenye umri wa miaka 23 ambaye anazuiliwa katika kambi moja kaskazini mashariki mwa Syria kutokana na kunyimwa uraia wake wa Uingereza, amesema: “Inaonekana kwamba ukusanyaji wa taarifa za kijasusi ni kipaumbele cha serikali ya Uingereza na wala serikali hii haijali kuhusu watoto.”

Shamima Begum aliyezaliwa na wazazi wa Bangladesh, aliondoka London mwaka 2015 alipokuwa na umri wa miaka 15 na kusafiri hadi Syria kupitia Uturuki pamoja na wasichana wengine wawili wa shule. Huko Syria, aliolewa na gaidi wa ISIS.

Begum alipatikana katika kambi ya wakimbizi mnamo 2019 ambapo serikali ya Uingereza ilibatilisha uraia wake na kutangaza kuwa alikuwa tishio la usalama.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *