Kan’ani: Kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni hakurejeshi utulivu na usalama Asia Magharibi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema “kuanzishwa uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na Kiislamu na utawala wa Kizayuni wa Israel hakutasaidia kuimarisha amani na usalama eneo la Asia Magharibi wala kudhamini haki za wananchi wa Palestina.”

Akijibu swali kuhusu hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, Nasser Kan’ani Chafi ameleza kuwa, msimamo wa Iran kuhusu utawala wa Kizayuni wa Israel na utambulisho wake haramu uko wazi na kuongeza kuwa: Tunaamini kwamba kuanzishwa na kustawisha uhusiano kati ya nchi za Kiarabu na Kiislamu na utawala huo hakutasaidia kuimarisha utulivu na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia na wala hakutasaidia kurejesha haki za watu wa Palestina. Ameongeza kuwa, taifa la Palestina linatarajia kuona nchi za Kiarabu na Kiislamu zikiunga mkono haki za taifa hilo kwa nguvu zao zote.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kwamba taifa la Palestina halikaribishi hatua yoyote ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na kuongeza kuwa: Mataifa ya eneo hili yameonyesha upinzani wao dhidi ya juhudi za kuanzishwa uhusiano kati ya baadhi ya nchi na serikali za Kiarabu na utawala wa Kizayuni.

Kan’ani Chafi amesema: Tunatumai kuwa mitazamo ya wananchi wa Palestina na mitazamo ya mataifa ya eneo hili itazingatiwa na tawala za Kiarabu na kwamba zitatilia maanani zaidi utambulisho halisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Matamshi hayo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yamekuja baada ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa serikali ijayo ya utawala wa Kizayuni, kueleza kwamba Tel Aviv inaendeleza juhudi za kuivuta Saudi Arabia kwenye kundi la nchi ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo.

Hadi sasa nchi nne za Kiarabu yaani Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zimeanzisha uhusiano wa wazi wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni kwa mashinikizo na upatanishi wa Marekani na bila ya kujali jinai na uhalifu unaofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina. Hatua hyo imekabiliwa na wimbi la upinzani wa nchi nyingi za Kiarabu na Kiislamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *