BAADA ya kipindi kirefu cha kutojulikana mrengo anaouegemea, hatimaye Kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua amejiunga na Azimio la Umoja na kutangaza atampigia debe Raila Odinga kwenye kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.
Bi Karua alitoa tangazo hilo jana baada ya kufanya mkutano wa faragha na Bw Odinga katika Serena Hotel, Nairobi.
“Niko hapa kuthibitisha kuwa, kuanzia sasa, Narc Kenya na mimi tunaunga mkono mgombeaji urais wa Azimio la Umoja, Raila Amolo Odinga,” Bi Karua akawaambia wanahabari.
“Jinsi nilivyosema awali, kama Narc Kenya tumekuwa tukikamia kufanya kazi na viongozi ambao wanaweka mbele masilahi ya taifa hili badala ya masilahi yao ya kibinafsi,” akaongeza.
Bi Karua alisema kuanzia sasa, atazunguka kote nchini akimfanyia kampeni Bw Odinga chini ya mwavuli wa vuguvugu la Azimio la Umoja.
Kabla ya kufikia uamuzi wa jana, kiongozi huyo wa Narc Kenya amekuwa mwenyekiti wa muungano wa viongozi wa Mlima Kenya (Mt Kenya Leader Forum) unaoshirikisha waziri wa zamani wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri, Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Spika wa Bunge la Kitaifa Justini Muturi.
Baadaye mapema mwaka huu 2022, Bi Karua alijiunga na muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na kuapa kushirikiana na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi na aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo.
Lakini alisalia kivyake kuanzia Machi 12, 2022 baada ya Mbw Musyoka, Gideon na Jirongo kujiunga na Azimio la Umoja katika hafla iliyoandaliwa katika jumba la KICC.
Siku moja kabla ya kuandaliwa kwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) la chama cha United Demcratic Alliance (UDA) katika uwanja wa Karasani, Nairobi, uvumi ulienea kuwa Bw Karua angehudhuria.
UDA
Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindi aliwaambia wanahabari kwamba, kiongozi huyo wa Narc Kenya ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ambako Naibu Rais William Ruto aliidhinishwa kwa mgombeaji urais wa UDA.
“Miongoni mwa wageni tunaowatarajia kuhudhuria mkutano wetu kesho (Machi 15) ni vinara wa ANC, Ford Kenya na kiongozi wa Narc Kenya,” Profesa Kindiki akawaambia wanahabari katika makao makuu ya UDA, Nairobi.Lakini dakika chache baadaye, Bi Karua alikanusha madai hayo kupitia akaunti yake ya Twitter kwa kusema, “Sio Kweli!”
Lakini Jumatatu wiki hii, kiongozi huyo wa Narc Kenya alisema bado anatafakari kuhusu ni mrengo upi atauunga mkono akidokeza kuwa atajiunga na upande ambao una “idadi ndogo ya watu wabaya.”
Hii ni baada ya Bw Kuria ambaye ni kiongozi Chama Cha Kazi (CCK) kumashauri kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza ili ateuliwe kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto.
Jana Jumatano, Bi Karua alirejelea kauli yake kwamba mirengo yote miwili ina watu wazuri na watu wabaya.
“Narudia kauli yangu ya awali kwamba, kila upande una watu ambao wamewahi kupora pesa za umma na kuendeleza utawala dhalimu na pia kuna watu wazuri ambao ni watetezi wa wanyonge. Lakini sasa nimejiunga na upande huu wa Azimio kwa sababu una idadi ndogo ya waporaji wa mali ya umma. Aidha, unaongozwa na mwenzangu katika ukombozi wa pili, Bw Raila Odinga,” akaeleza.
Kwa upande wake, Bw Odinga alisema alikuwa na matumaini makubwa kwamba, Bi Karua angemuunga mkono na wala sio mpinzani wake mkuu Dkt Ruto.
“Sidhani kwamba, alikuwa na chaguo jingine, kwa sababu tofauti kati ya upande huu na upande ule mwingine (wa Dkt Ruto) ni kama usiku na mchana; nyeusi na nyeupe,” akasemaBw Odinga akimtaja Bi Karua kama shujaa wa ukombozi wa pili wa taifa hili na mshirika wake mkuu katika mapambano yaliyoleta ukombozi huo katika miaka ya 90s.
“Mimi na dadangu Karua tulipitia wakati mgumu zaidi wakati wa ukombozi wa pili wa taifa hili. Leo nimefurahi kwamba tumeungana tena kuleta ukombozi wa tatu wa kiuchumi kwa manufaa ya Wakenya wote,” Bw Odinga akasema.
Hatua ya kiongozi huyo wa Narc Kenya kujiunga na Azimio la Umoja ni faida kubwa kwa Bw Odinga ambaye anasaka uungwaji mkono kutoka eneo la Mlima Kenya.
Wadadisi wanasema hatua hiyo sasa inamweka Bi Karua katika nafasi bora ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga. Hii ni licha ya kwamba, amejitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kirinyaga.