Katibu Mkuu wa Hizbullah amsifu Jenerali Soleimani kama ‘Kiongozi Mkuu’ katika mapambano dhidi ya Daesh na Israel

Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon amepongeza kujitolea mhanga kwa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, akisema kamanda huyo mashuhuri alikuwa “Kiongozi Mkuu” aliyelishinda kundi la kigaidi la Daesh na kuuzuia utawala wa kigaidi wa Israel kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na Walebanon.

Sayyed Hassan Nasrullah aliyasema hayo siku ya Jumanne katika hotuba ya televisheni kutoka Dahiyeh kusini mwa mji mkuu wa Lebanon Beirut, wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka wa tatu wa kuuawa shahidi Jenerali Soleimani katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani nchini Iraq, na kujadili matukio mengine ya hivi karibuni nchini Lebanon na eneo zima la Asia Magharibi.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyopewa jina la ‘Tuzo la Kimataifa la Soleimani kwa Fasihi ya Upinzani,” Nasrullah amesema kamanda huyo mkuu amepita mipaka ya wakati na mahali, na si wa Iran pekee bali ni wa mataifa yote.

Nasrullah amesema sifa muhimu zaidi ya Jenerali Soleimani ni “nguvu zake za kimaadili na ujasiri usio na kifani” ambao uliwatia moyo wale wote waliofanya kazi naye.

Katibu Mkuu huyo wa Hizbullah amesema Jenerali Soleimani alikuwa na uwezo mkubwa wa kuvutia vizazi vijavyo, na kwamba ni wajibu wetu kukumbuka na kulea shakhsia na mashahidi kama yeye.

Amesema katika kila kizazi, tunahitaji kuwa na mifano kama hawa mashahidi, ambao wako katika kila uwanja wa vita, na ambao majina yao lazima yahuishwe kwani yanawakilisha utajiri mkubwa wa kiakili na kiroho ambao hatupaswi kuudharau.

Akiashiria ombwe la urais nchini Lebanon, Nasrullah ameashiria mashinikizo ya nje na ndani yanayozuia na kuchelewesha kuchaguliwa rais wa nchi hiyo inayokumbwa na mgogoro wa kisiasa na kiuchumi.

Ameashiria tatizo la nishati nchini humo na kusema: “Kila mtu nchini Lebanon anakabiliwa na tatizo la umeme na mafuta ambalo ni kubwa zaidi kuliko tofauti za kidini na kimakundi, na athari zake zimeathiri pakubwa uchumi na maisha ya kawaida ya watu.”

Amesema: “Miezi kadhaa iliyopita, tuliambiwa tuagize mafuta kutoka Iran kwa muda wa miezi 6, tuongeza saa za usambazaji wa umeme hadi saa 8 na kuiweka Lebanon kwenye njia ya kupata suluhisho. Tulichukua hatua na kuwasiliana na Iran, na walikubali ombi la kuipa Lebanon mafuta. Ofa ya mafuta ya Iran kwa Lebanon bado ipo lakini ni Wamarekani ndio wanazuia utekelezaji wake.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *