Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mauaji ya raia huko Gaza na kutaka pande husika zijizuie

Jumla ya Wapalestina 20 wakiwemo wanawake wasiopungua watano na watoto watano wameuawa shahidi tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel kabla ya mapambazuko siku ya Jumanne.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Farhan Haq, naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, alisema Katibu Mkuu wa shirika hilo, Antonio Guterres, alitaja mauaji ya raia huko Gaza kuwa “hayakubaliki” na kuzitaka pande husika “kusimamisha ghasia mara moja” na kwamba pande zote zinapaswa kujizuia kwa kiwango cha juu.
Siku ya Jumatano, kwa siku ya pili, utawala wa Kizayuni ulishambulia malengo ya Jihad ya Kiislamu na makundi ya muqawama huko Ghaza, na pia kurusha mamia ya maroketi katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, na kengele za hatari zikasikika hata mjini Tel Aviv. Wakati huo huo, Misri imeanza juhudi za upatanishi ili kumaliza migogoro hiyo.
Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walikutana kwa faragha siku ya Jumatano ili kujadili maendeleo ya hivi punde kuhusiana na mgogoro huu.
Maafisa wa afya wa Palestina wametangaza kuwa, tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel kabla ya alfajiri ya Jumanne, jumla ya Wapalestina 20, wakiwemo wanawake wasiopungua watano na watoto watano, pamoja na makamanda watatu wakuu wa Islamic Jihad na watu wanne waliokuwa na silaha, wameuawa shahidi.

Kuhusiana na suala hilo, Farhan Haq amesema: “Israel lazima ifuate wajibu wake kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu sawia na kupitishwa kwa tahadhari zote zinazowezekana ili kuhifadhi (maisha) ya raia na mali za raia wakati wa operesheni za kijeshi.”
Farhan Haq, bila kugusia haki zisizopingika za Wapalestina za kujitetea, alisema kuwa Guterres pia analaani urushaji wa maroketi kiholela kutoka Gaza kuelekea maeneo ya Israel na kwamba kitendo hicho kinakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.
“Katibu Mkuu anatoa wito kwa pande zote zinazohusika kutekeleza kiwango cha juu cha kujizuia na kujitahidi kukomesha uhasama mara moja,” ilisema taarifa ya Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *