Katika uamuzi wa aina yake.. Rais wa zamani wa Ufaransa ahukumiwa kifungo miaka 3 jela katika kesi ya ufisadi

Mahakama ya Rufaa ya Paris leo, Jumatano, imemhukumu Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy kifungo cha miaka 3 jela, ambapo anawekwa chini ya uangalizi kwa kufungwa bangili ya kielektroniki. Ni baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na ufisadi na kutumia vibaya madaraka, hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya rais wa zamani wa Ufaransa.

Mahakama ya Rufaa ya Paris ilimepasisha uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Mwanzo mnamo Machi 1, 2021 dhidi ya rais huyo wa zamani wa mrengo wa kulia, ambaye alisikiliza uamuzi huo akiwa ameketi kwenye benchi za washtakiwa.

Nicolas Sarkozy, 68, anakuwa rais wa kwanza wa zamani wa Ufaransa kuhukumiwa kifungo, baada ya mtangulizi wake, Jacques Chirac, kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kilichosimamishwa mwaka 2011 katika kesi ya kazi ya uongo huko Paris.

Mahakama hiyo ya Rufaa pia imetoa hukumu nyingine mbili zinazompokonya Sarkozy haki zake za kiraia kwa kipindi cha miaka 3, jambo ambalo linamyima ustahiki wa kushiriki katika uchaguzi wowote.

Nicolas Sarkozy, ambaye alishika wadhifa wa Rais wa Ufaransa kuanzia 2007-2012, amepinga vikali uamuzi huo.

Sarkozy atafikishwa tena katika Mahakama ya Rufaa katika msimu wa vuli kwenye kesi ya ufadhili haramu wa kampeni yake ya urais 2012. Vilevile anakabiliwa na hatari ya kufunguliwa kesi ya tatu, baada ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Taifa  Alhamisi iliyopita kuomba afikishwe kwenye Mahakama ya Jinai katika kesi ya tuhuma za ufadhili wa kifedha aliopata kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi kwa ajili ya kampeni yake ya uchaguzi wa rais mwaka 2007.

Ni vyema kutambua kwamba Nicolas Sarkozy ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, alijulikana kwa uaminifu wake mkubwa kwa Marekani na utawala haramu wa Israel.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *