Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amemwita waziri mkuu wa India Narednra Modi “Chinjachinja wa Gujarat” baada ya waziri mwenzake wa India kuishutumu Pakistan kuwa “kitovu cha ugaidi” huku majirani hao wenye silaha za nyuklia wakikabiliana kwa vita vya maneno katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Majibizano makali kati ya Bilawal Bhutto-Zardari wa Pakistan na Subrahmanyam Jaishankar wa India yalikuja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha taarifa jana Alkhamisi ya kuonya juu ya hatari inayoongezeka ya ugaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo wa Umoja wa Mataifa, Waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar aliita Pakistan “kitovu cha ugaidi”.
“Ushauri wangu ni kujisafisha na kujaribu kuwa jirani mwema,” alisema Jaishankar.
Awali kabla ya hapo na bila kuitaja Pakistan kwa jina, Jaishankar, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba “India ilikabiliwa na hali ya kutisha ya ugaidi wa kuvuka mpaka muda mrefu kabla ya ulimwengu kuchukua tahadhari” na “imepambana na ugaidi kwa uthabiti, kwa ujasiri na kwa mtazamo usio na uvumilivu” .
Wakati Bhutto-Zardari alipoulizwa ili kujibu madai ya Jaishankar, alisema, Wahindi wanaendelea kusema “Muislamu na gaidi ni kitu kimoja”, aweko Pakistan au India.
Mwanadiplomasia mkuu huyo wa Pakistan alisema Jaishankar anapaswa kukumbuka kwamba “Osama bin Laden amekufa, (lakini) chinjachinja wa Gujarat angali anaishi na yeye ni waziri mkuu wa India”.
Waziri Mkuu Mhindu wa India Narendra Modi alikuwa waziri kiongozi wa jimbo la Gujarat wakati wa machafuko ya kidini mwaka 2002 yaliyoua karibu watu elfu mbili akthari yao wakiwa ni Waislamu.
Modi alishutumiwa kwa kufumbia macho vurugu hizo. Hadi kuchaguliwa kwake kama waziri mkuu mwaka wa 2014, alikuwa amekataliwa kuingia Marekani.