Wakili na mwanaharakati Miguna Miguna hatimaye amewasili nchini mapema Alhamisi.
Bw Miguna ana uraia wa nchi mbili; Kenya na Canada, na alitimuliwa nchini na serikali ya Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta 2018 baada ya vuta nikuvute alipomuapisha Raila Odinga kama ‘Rais wa Wananchi’.
Alikuwa mmoja wa mawakili waliomuapisha kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa ‘Rais wa Wananchi’ mapema mwaka aliofurushwa baada ya kushindwa na Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu 2017.
Kosa la aina hiyo linatafsiriwa kama ukiukaji wa sheria na Katiba ya nchi, adhabu yake ikiwa kunyongwa.
Bw Odinga na Rais Kenyatta hata hivyo Machi 2018, walizika tofauti zao kisiasa chini ya salamu za maridhiano, almaarufu Handisheki wawili hao wakishirikiana kuendesha serikali, urafiki ambao Miguna Miguna alidai ulichangia masaibu yake.
Wakili huyo aidha alikuwa amebuni vuguvugu la National Resistance Movement (NRM), lililoharamishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani anayeondoka, Dkt Fred Matiang’i.
Alifanya majaribio kadha kurejea nchini, japo hakufua dafu.
“Ninaridhia makaribisho ya dhati na upendo mlioonyesha (akimaanisha waliomlaki na wafuasi wake) kunikaribisha tena katika nchi yangu,” Bw Miguna akasema akihutubia wanahabari katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi baada ya kutua kutoka Canada.
Akizungumza, alionekana mwenye ujasiri na ukakamavu.
Mwanaharakati huyo alieleza kuridhishwa kwake na serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt William Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua akisema ‘isingekuwa utawala huu mpya asingerejea nchini’.
Hali kadhalika, aliishukuru idara ya mahakama kwa kile alisisitiza ilisimamia haki na ukweli ikimtetea kurejea taifa alilozaliwa.
“Yaliyonitendekea hayapaswi kufanyikia mtu mwingine yeyote yule…Mzaliwa wa Kenya hawezi kutolewa kimabavu na kutupwa ugenini.”
Alipakia Jumatano jioni kwenye akaunti zake za mitandao; Twitter na Facebook, ratiba ya Alhamisi baada ya kuwasili.
Anahudhuria maadhimisho ya Mashujaa Dei, na pia amepata mwaliko Ikulu ya Rais Nairobi.