Kenya miongoni mwa nchi zitakazoanza kutengeneza chanjo za Covid-19 kwa teknolojia ya mNRA

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, nchi sita za Afrika zimechaguliwa kuanza utengenezaji wao wa chanjo za Covid-19 kwa kutumia teknolojia ya mfumo wa mRNA.

Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Senegal, Misri na Tunisia zimechaguliwa kuwa nchi za kwanza kupokea teknolojia ya mRNA kutoka kituo Shirika la Afya Duniani (WHO) cha kimataifa, katika bara hilo ambalo, kwa kiasi kikubwa limeendelea kukabiliwa na changamoto za upatikanaji wa chanjo za ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa WHO ni kuwa, hatua hiyo ni katika msukumo wa kuhakikisha Afrika inaweza kujitengenezea chanjo zake za kupambana na Covid na magonjwa mengine.

Hafla ya Sherehe ya kutangaza uhamishaji wa teknolojia hiyo ya mRNA ilitarajiwa kufanyika jana Ijumaa mjini Brussels, Ubelgiji, katika mkutano wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.

Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amesema kuwa, hakuna tukio lingine kama janga la Covid-19 ambalo limeonyesha kuwa, kutegemea makampuni machache kusambaza bidhaa za afya ya umma ulimwenguni ni hatari.

Ameongeza kuwa teknolojia inayoleta mapinduzi ya mRNA hufundisha seli za mwili jinsi ya kutengeneza protini ambayo huchochea mwitikio wa kinga, bila kutumia nyenzo yoyote ya virusi.

Kituo cha kimataifa cha uhamishaji wa teknolojia cha mRNA kilianzishwa nchini Afrika Kusini mwaka jana ili kusaidia nchi za kipato cha chini na cha kati katika kutengeneza chanjo zao za mRNA kwa taratibu za uendeshaji zinazohitajika na ujuzi wa kufikia viwango vya kimataifa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *