Kenya; Rais Mteule Azungumza Na Rais Mstaafu

Rais Mteule Dkt William Ruto hatimaye amezungumza na Rais anayeondoka, Uhuru Kenyatta kuhusu mikakati kutwaa serikali namna alivyoahidi Wakenya kwenye hotuba yake kwa taifa Mahakama ya Upeo ilipoidhinisha ushindi wake mnamo Jumatatu, Septemba 5, 2022.

Mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga alikuwa amepinga mahakamani matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 na ambayo yalitangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati.

“Nitampigia simu Rais Kenyatta, hatujazungumza kwa muda wa miezi kadhaa. Tutajadiliana kuhusu mikakati ya mpito,” Ruto akaahidi mnamo Jumatatu.

Na leo Jumatano Rais huyo mteule ametangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwamba kweli amezungumza na mkubwa wake huyo wa tangu mwaka 2013 walipoingia serikalini.

“Kwa njia ya simu, nimezungumza na bosi wangu, Rais Uhuru Kenyatta. Tulijadiliana kuhusu uchaguzi mkuu wa hivi punde, na mikakati ya mpito kama ilivyo kwa mujibu wa demokrasia yetu na mazoea,” Dkt Ruto akaandika.

Rais Kenyatta kwenye hotuba yake kwa taifa baada ya maamuzi ya korti, aliahidi kupokeza mamlaka kwa mshindi na mrithi wake.

Mipango ya mpito inaendelea, hafla ya kitaifa ikitarajiwa kufanyika Jumanne Septemba 13, katika uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani jijini Nairobi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *