Kenya yawawinda wanaoeneza chuki kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa ya Kenya (NCIC), inachunguza watu 51 kwa tuhuma za kusambaza matamshi ya chuki huku kaunti sita zikikihofiwa kukumbwa na vurugu za kisiasa katika kipindi hiki nyeti cha kampeni kali za kuwapigia debe wanasia wanaowania kiti cha rais wa nchi hiyo.

Mwenyekiti wa NCIC, Samuel Kobia, amesema watu 36 walichapisha kauli za chuki kwenye mitandao ya kijamii huku wengine 15 wakitoa kauli kama hizo kwenye mikutano ya kisiasa. Amesema kuwa Kinara wa ODM, Raila Odinga na mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ni miongoni mwa wanasiasa wanaochunguzwa kwa madai ya kutoa matamshi yanayoaminika kuwa ya chuki.

Baadhi ya kaunti zilizotajwa kuwa huenda zikakumbwa na vurugu za kisaiasa ni Migori, Homa Bay, Kisumu, Nandi, Kericho na Nakuru. Dkt Kobia amesema, “Nataka kuwahakikishia Wakenya kuwa visa vyote vya matamshi ya chuki vitachunguzwa. Kila mmoja anatawaliwa kufuata sheria kwa hivyo, hakuna aliye juu ya sheria.”

Kadhalika, amesema kuwa tume hiyo itachapisha baadhi ya maneno ya chuki kwa lugha zote na maneno hayo kupigwa marufuku katika hafla zote za kampeni kama njia ya kudumisha amani na umoja kadiri uchaguzi unavyokaribia.

 Mwenyekiti wa NCIC amesema: “Maneno kama vile ‘madoadoa’ hasa katika hafla za kisiasa yanasababisha utengano na chuki katika jamii hasa zinazotoka mipakani. Vigogo vya kisiasa waepuke maneno kama hayo. Uchaguzi mkuu wa Kenya umepangwa kufanyika tarehe 9 Agosti mwaka huu wa 2022.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *