Khalid Mash’al: Kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni ni kulisaliti taifa la Palestina

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS nje ya nchi amesema mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ni kosa kubwa na usaliti kwa taifa la Palestina.

Faraan: Khalid Mash’al ameeleza kuwa, nyenzo na suhula zote, kuanzia muqawama na upinzani wa umma pamoja na kuendesha mapambano kwa mtutu wa bunduki, ni halali kisheria kutumiwa na Wapalestina kwa ajili ya kupata haki zao.

Mash’al amesema, mikataba ya mapatano iliyosainiwa na nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel haijawa na tija wala faida yoyote na akaongeza kwamba, kueneza fikra ya kufanya mapatano na utawala ghasibu unaokalia ardhi kwa mabavu na kutaka kuonyesha kuwa utawala huo ni rafiki katika eneo la Asia Magharibi hakuwezi kubadilisha uhakika wa mambo.

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina nje ya nchi amesisitiza kuwa, taifa la Palestina litaendeleza muqawama na mapambano yake dhidi ya Israel ili kuhakikisha linapata haki zake na linakomesha kukaliwa kwa mabavu ardhi yake na mwishowe litapata ushindi.

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan ni nchi za Kiarabu zilizochukua hatua katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita ya kupatana na Israel ili kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu wa Kizayuni unaokikalia kwa mabavu kibla cha kwanza cha Waislamu.

Kwa zaidi ya miongo saba sasa tangu ulipoivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina, utawala ghasibu wa Kizayuni umeshakanyaga mara kadhaa haki za Wapalestina, mbali na kutenda kila aina ya jinai dhidi ya wamiliki hao wa asili wa ardhi hiyo.

Hadi sasa utawala bandia wa Israel ungali unaendeleza sera za ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina, kuwatoa na kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina katika nyumba zao na kuuwekea mzingiro wa kidhalimu Ukanda wa Gaza…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *