Khiyana zingine mbili za Imarati dhidi ya Palestina

Isaac Herzog, Rais wa utawala haramu wa Israel Jumatatu alasiri aliwali Abu Dhabi mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarat) ikiwa ni safari yake ya pili katika nchi hiyo kwa mwaka huu wa 2022.

Herzog pamoja na mambo mengine amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Imarati Mohmammad bin Zayed al-Nahyan. Rais wa Israel aliwasili Abu Dhabi akitokea Bahrain katika safari iliyokabiliwa na upinzani mkali na maandamano makubwa ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu wanaopinga nchi yao kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv.

Imarati imemkaribisha Rais wa utawala ghasibu wa Israel katika mazingira ambayo nchi hiyo imekuwa ikisitiza kuendelea kuwa na uhusiano na utawala huo bandia unaokabiliwa na malalamiko ya walimwengu kutokana na kutenda jinai dhidi ya Wapalestina.

Safari hiyo inafanyika katika hali ambayo, ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu umeendelea kushuhudia malalamiko na maandamano ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel. Kilele cha upinzani huo kimeshuhudiwa katika mashindano ya soka ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar.

Wakati wa michezo ya Kombe la Dunia huko Qatar, raia wa nchi tofauti za Kiarabu sio tu wamekataa kuzungumza na vyombo vya habari vya Israel, bali wamekuwa wakiliunga mkono wazi wazi taifa la Palestina, na hata mchezaji wa Morocco Jawad Elyamiq alinyanyua bendera ya Palestina na kuiweka begani baada ya ushindi wa Morocco dhidi ya Canada.

Hatua ya Imarati ya kumkaribisha Rais wa Israel katika nchi yake na kumtandikia zulia jekundu inahesabiwa kuwa khiyana na usaliti mwingine wa nchi hiyo kwa Palestina na wananchi wa taifa hilo madhulumu wanaotaabika kwa masaibu ya kila namna. Mbali na usaliti huo, katika khiyana nyingine, utawala wa Imarati ulimualika Itamar Ben Gvir, kiongozi wa chama cha Kiyahudii na mmoja wa shakhsia wenye misimamo ya kufurutu mpaka katika ubalozi wake mjini Tel Aviv kwa mnasaba wa miaka 50 ya kujipatia uhuru.

Akihutubia katika maadhimisho hayo ya uhuru wa Imarati, Mzayuni huyo mwenye misimamo ya kuchupa mipaka alisema: Tunaweza kufikia mapatano na Waarabu bila ya kusalimu amri wala kuwapa fursa za upendeleo. Ninatoa mkono wa pongezi kwa Imarati kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya taifa ya nchi hiyo na nimefurahi mno kushiriki katika hafla hii hapa kwenye ubalozi wa Imarati mjini Tel Aviv. Hii ndio suluhu na mapatano ya kweli.

Muhammad Ali al-Khaja, balozi wa Imarati huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu hakutoa radiamali yoyote kwa matamshi hayo ya Itamar Ben Gvir na badala yake alisisitiza tena juu ya kuendelezwa uhusiano wa nchi yake na Israel na kueleza kwamba, Israel na Imarati zimeanza kuandika matukio ya kihistoria na hii siyo ndoto au kuwa usingizini.

Wakati Imarati ilipotiliana saini makubaliano na Israel ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao, ikiwa na lengo la kuonyesha kwamba, makubaliano hayo hayako kinyume na maslahi ya Wapalestina ilikuwa ikidai kuwa, imepatia dhamana ya lazima ya kutounganishwa bonde la Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.  Hii ni katika hali ambayo, serikali mpya ya Israel na shakhsia wake muhimu kama Ben Gvir siyo tu kwamba, hawatotosheka na kuunganishwa bonde hilo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu bali wamo mbioni kuunda makundi ya wanamgambo wa Kizayuni ambao kazi yao itakuwa ni kuwatimua Wapalestina ambao ni wakazi wa ukingo huo.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana wananchi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu wameendelea kupinga vikali hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel hasa kutokana na kuwa, hatua hiyo haina maslahi hata kidogo kwa wananchi wa Palestina na malengo yao ya kujikomboa na kujiamulia hatima na mustakabali wao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *