Jana Jumamosi, ulifanyika uchaguzi nchini Bahrain wa kuchagua wabunge 40 wa Baraza la Wawakilishi na wajume 30 wa Mabaraza ya Miji.
Wakati huo huo, serikali inayotawala Bahrain, kupitia muswada uliopitishwa mwaka 2018, wakati nchi hiyo ilipokuwa ikichukua hatua za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa mashinikizo ya serikali ya Trump na kwa baraka kamili za Saudi Arabia, iliwanyang’anya uraia Wabahrian wengi na kupiga marufuku shughuli za vyama na makundi ya kisiasa ya upinzani, na hivyo kuwanyima haki yao wananchi hao ya kushiriki katika uchaguzi. Sambamba na hatua hiyo, serikali ya Manama iliwapatia uraia, raia wengi wa Kisunni kutoka nchi mbalimbali na hasa wenye imani za kitakfiri ambao walishiriki katika vita vya Syria ili kufanikisha mpango wa kuipindua serikali ya nchi hiyo. Kwa kuwapatia uraia watu hao, utawala wa kifalme wa aila ya Aal Khalifa uliwaandalia mazingira ya kupiga kura katika uchaguzi wa jana.
Kwa kuzingatia kwamba kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ubaguzi mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Bahrain tangu kuasisiwa kwa nchi hiyo, tunaweza kusema kuwa, moja ya sifa maalumu za uchaguzi bandia wa Novemba 12 ni kuwa kwake uchaguzi wa kwanza kufanyika baada ya utawala wa Aal Khalifa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel; na hiyo ni sababu moja kuu ya ususiaji mkubwa wa uchaguzi huo uliofanywa na vyama na makundi ya wananchi, kama ambavyo kwa sehemu kubwa, utawala wa Manama umefanya kila njia ili kuupatia uhalali wa kisheria uchaguzi huo wa jana kutokana na suala hilohilo la kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala bandia wa Israel.
Hivi sasa Bahrain imekuwa tegemezi zaidi kwa Saudi Arabia, na kwa kujiweka karibu na utawala wa Kizayuni, imeathiriwa pia na mielekeo ya utawala huo haramu katika siasa zake za ndani; na ndio maana inaonekana ikiiga na kufuata kikamilifu mbinu zile zile ambazo kwa miongo kadhaa sasa zimekuwa zikitumiwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina, ikiwemo kuwavua uraia wakazi wa asili wa Bahrain na kuwapatia uraia watu ambao hawana asili yoyote ya nchi hiyo.