Makumi ya watu wamepoteza maisha huku mamilioni ya wengine wakiathiriwa moja kwa moja na kimbunga kikali kilichokumba majimbo kadhaa ya Marekani wakati huu wa msimu wa baridi kali.
Maafisa nchini humo wamesema akthari ya vifo 28 vilivyoripotiwa kufikia sasa vimetokana na baridi kali, ajali za barabarani, kuanguka kwa miti na athari nyingine zilizosababishwa na kimbunga hicho kilichopewa jina la ‘Kimbunga cha Bomu’.
Athari za janga hilo la kimaumbile zimepelekea nyumba zaidi ya milioni moja na laki nane kukatikiwa na umeme, huku maelfu za safari za ndege zikifutwa au kuakhirishwa.
Majimbo yaliyoathirika zaidi na kimbunga hicho ni Kentucky, Missouri, Oklahoma na Ohio. Majimbo mengine yanayokabiliwa na matatizo chungu nzima wakati huu wa baridi kali ni pamoja na Tennesee, Pennsylvania, Carolina Kaskazini, na Vermont.
Taarifa kutoka New York mji ambao umeshuhudia upepo mkali ulioambatana na theluji zinasema kuwa, idara za uokoaji zimelemewa katika kushughulikia dharura, huku uwanja wa ndege wa kimataifa kwenye mji huo ukifungwa kwa muda, na yumkini ukafunguliwa kesho Jumatatu.
Baadhi ya majimbo nchini Marekani kama Montana yamenakili baridi shadidi yenye kiwango cha nyuzijoto 45 chini ya daraja, huko jimbo la Ohio likirekodi kiwango hasi cha 38.
Hii ni katika hali ambayo, jarida la Economist hivi karibuni lilitoa indhari na kusema kuwa, kuna uwezekano wa kutokea vifo 147,000 katika msimu huu wa baridi kali huko Ulaya, kwa kuzingatia kupanda kwa bei ya nishati. Aidha iwapo baridi itaongezeka na kuwa kali zaidi, idadi ya vifo itafikia 185,000 katika bara hilo linalokabiliwa na mgogoro wa nishati.