Kimya cha jamii ya kimataifa na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina

Mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya raia wa Palestina yanaendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu katika kivuli cha kimya na upuuzaji wa jamii ya kimataifa.

Mashambulizi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni yameshtadi katika miezi kadhaa ya karibuni katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hasa katika miji ya Jenin na Nablus; ambapo makumi ya Wapalestina wameuliwa shahidi na mamia ya wengine kujeruhiwa katika hujuma hizo za wanajeshi wa Israel.

Katika kuendelea mashambulizi hayo, juzi Alhamisi pia wanajeshi wa Kizayuni waliivamia kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Jenin kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambapo vijana wawili wa Kipalestina waliuawa shahidi na watatu kujeruhiwa. Wanajeshi wa Israel jana asubuhi pia waliushambulia mji wa Nablus na kumjeruhi Mpalestina mmoja.

Kuna sababu mbalimbali kuhusu kuendelea jinai hizo tajwa za Wazayuni.

Inaonekana kuwa katika mazingira ya sasa sababu kuu ni kustafidi na fursa ya mashindano ya Soka la Kombe la Dunia yanayoendelea huko Qatar. Fikra za walimwengu duniani hivi sasa zimejielekeza katika mashindano hayo ya Kombe la Dunia huko Qatar. Utawala wa Kizayuni siku zote umeonyesha namna unavyotumia masuala yanayozishughulisha na kuvutia fikra za waliowengi duniani kama fursa ya kutekeleza siasa zake za kupenda kujitanua na mabavu  dhidi ya Wapalestina.

Sababu nyingine ya Wazayuni kushadidisha vitendo vyao vya mabavu ni kutokana na kuwa wametambua namna fikra za waliowengi zilivyo dhidi yao katika eneo. Katika mashindano hayo ya dunia imebainika wazi kwamba, fikra za waliowengi na khususan katika Ulimwengu wa Kiarabu ziko dhidi ya utawala wa Kizayuni; na utawala huo unaghadhibishwa sana na suala hilo. Oren Hasson Rais wa Shirikisho la Soka la utawala wa Kizayuni amesema kuhusu tajiriba mbaya na isiyoridhisha iliyowakumba maripota na waandishi habari wa vyombo vya habari vya lugha ya Kiibrenia katika Kombe la Dunia huko Qatar kwamba: “Imenibainikia kuwa, Waisraili wanachukiwa huko Qatar. Ni wazi  kuwa, Wazayuni wanatoa hasira zao kwa Wapalestina.

Sababu nyingine ni hii kuwa, utawala wa Kizayuni na hasa katika miaka miwili ya hivi karibuni umefikia natija hii kwamba, kwa utulivu kabisa unaweza kutekeleza siasa zake za ukandamizaji kuhusu Wapalestina. Wakati huo huo madola makubwa duniani yamenyamaza kimya na kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina na nchi za Kiarabu katika miaka miwili ya karibuni zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu na kudhihirisha kimya chao mbele ya jinai hizo za kila uchao za Wazayuni huku zikiridhika tu na kuchukua hatua ya kutoa matamshi ya kulaani jinai hizo. Kuhusiana na hilo, Bunge la Kiarabu limelaani hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuzidisha mivutano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kutahadharisha juu ya kuripuka hali ya mambo ambayo ni tishio kwa amani na usalama katika eneo.

Sababu nyingine kuu inahusiana na kuwa macho na kusimama imara makundi ya muqawama ya Palestina na kufikia natija hii kuwa, njia pekee ya kukabiliana na jinai za Wazayuni ni kuendesha muqawama. Hasa ikizingatiwa kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja wa karibuni makundi ya Palestina yametekeleza oparesheni nyingi za kimuqawama dhidi ya Wazayuni zikiwemo zile zilizotekelezwa ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Utawala wa Kizayuni unakariri jinai zake ili kuzuia kuendelea oparesheni mbalimbali za kimuqawama.

Tel Aviv inadhani kwamba, jinai zake za kila uchao zinaweza kusitisha oparesheni za makundi ya kimuqawama za Wapalestina lakini fikra hiyo ni potofu. Hii ni kwa sababu, kwa upande mmoja, kuongezeka oparesheni za wanamapambano wa Palestina ni matokeo ya jinai za kila siku za utawala huo ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu; na kwa upande mwingine, makundi mbalimbali ya Palestina yamekubaliana kutekeleza oparesheni hizo za muqawama dhidi ya Wazayuni maghasibu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *